settings icon
share icon
Swali

Je! Wakristo wanapaswa kuwatizama waraibu wa pombe namna gani? Je! Biblia inasema nini kuhusu walevi?

Jibu


Uraibu wa pombe ni mojawapo ya uraibu mwingi unaoweza kudhibiti maisha ya mtu. Kwa sababu madhara yake ni dhahiri, ulevi unaweza kuonekana kuwa dhambi mbaya sana kuliko zingine. Hata hivyo, Biblia haijaweka tofauti hizo. Mara nyingi inalinganisha dhambi ya ulevi na dhambi tunazoweza kuzichukulia kuwa “zisizo muhimu,” kama vile wivu na tamaa ya ubinafsi (Wagalatia 5:19; 1 Wakorintho 6:10). Ni rahisi kuhukumu mtu ambaye anaanguka chini kwa kulewa, huku ukitoa udhuru kwa dhambi za siri za moyoni ambazo Mungu anaona ni za kuchukiza vile vile. Jibu sahihi ni kuwatizama watu jinsi na namna Mungu anavyowaona na kukubaliana naye kwamba sisi sote ni wenye dhambi na tunahitaji kuokolewa.

Biblia iko wazi kwamba ulevi ni dhambi (Isaya 5:11: Mithali 23:20-21; Habakuki 2:15). Mithali 20:1 inasema, “Mvinyo ni mdhihaki na kileo ni mgomvi; yeyote apotoshwaye navyo hana hekima.” Waefeso 5:18 inasema, “Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho.” Inashangaza kwamba mstari huu unatofautisha nguvu ya pombe na nguvu ya Roho Mtakatifu. Unasema kwamba ikiwa tunataka kutawaliwa na Roho wa Mungu hatuwezi pia kutawaliwa na pombe. Hawa wawili hawawezi kushikamana kwa pamoja. Tunapomchagua mmoja tunaondoa ushawishi wa mwingine. Kama Wakristo, tunapaswa “kuenenda katika Roho” daima (Wagalatia 5:16, 25; Warumi 8:1, 14). Kwa hiyvo ulevi kwa Mkristo kamwe haupaswi kuwa chaguo katika tukio lolote kwa sababu hakuna wakati ambapo hatupaswi kutembea katika Roho.

Ulevi ni aina ya sanamu, kama vile uraibu wowote ule. Chochote tunachotumia badala ya Mungu ili kukidhi au kuponya mahitaji ya ndani ya moyo ni sanamu. Tunapojitegemea sisi wenyewe, mtu mwingine, au kitu kingine ili kukidhi mahitaji yetu kwa thamani au umuhimu, tumesimamisha sanamu ambayo inachukua nafasi ya Mungu halisi katika maisha yetu. Mungu anaichukulia vivyo hivyo na ana maneno makali dhidi ya wanaoabudu sanamu (Kutoka 20:3; 34:14; 1Yohana 5:21; 1Wakorintho 12:2). Ulevi ni chaguo. Mungu anatuka tuwajibike kwa uchaguzi wetu (Warumi 14:12; Mhubiri 11:9; Waebrania 4:13).

Wafuasi wa Kristo wanapaswa kujitahidi kuwapenda majirani wao kama vile wanavyojipenda, bila kujali matatizo au uraibu ambao majirani hao wanaweza kuwa nao (Mathayo 22:29). Lakini kinyume na wazo letu la kisasa ambalo linalinganisha upendo na uvumilivu, upendo wa kweli hauvumilii au kutoa udhuru dhambi yenyewe ambayo inamwangamiza mtu (Yakobo 5:20). Kuwezesha au kutoa udhuru kwa uraibu wa pombe kwa mtu tunayempenda ni kushiriki kimyakimya katika dhambi zao.

Kuna njia nyingi Wakristo wanaweza itikia kwa upendo upendo wa Kikristo kwa waraibu wa pombe:

1. Tunaweza kuwahimiza waraibu wa pombe katika maisha yetu kupata msaada. Mtu aliyenaswa katika mtego wa uraibu anahitaji usaidizi na anawajibikaji. Kunayo mifumo mingi ya Kikristo ya urekebisho kama vile Celebrate Recovery (Sherehekea Kupona) ambayo inasaidia maelfu ya watu kujinasua kutoka kwa minyororo ya uraibu.
2.Tunaweza kuweka mipaka ili kutoruhusu ulevi kwa njia yoyote ile. Kupunguza matokeo ambayo matumizi mabaya ya pombe yanaweza kuleta haisaidii. Wakati mwingine njia pekee ya waraibu ya kutafuta usaidizi ni wakati wamefika mwisho wa chaguzi zao.
3. Tunapaswa kuwa waangalifu tusiwafanye wengine kujikwaa kwa kupunguza matumizi yetu ya pombe tukiwa pamoja na wale wanaosumbuliwa nayo (1 Wakorintho 8:9-13). Ni kwa sababu hii kuwa Wakristo wengi wanachagua kujiepusha na matumizi yote ya pombe ili kuepuka kuonekana na uovu wowote (1 Wathesalonike 5:22) na kutoweka kikwazo katika njia ya mwingine. Ni lazima tutathmini uhuru wetu dhidi ya uwezekano wa kuwasababisha wengine kufanya dhambi au kuwachanganya marafiki wanaohusisha pombe na maisha yao ya dhambi.

Ni lazima tuonyeshe huruma kwa kila mtu, ikiwa ni pamoja na wale ambao uchaguzi wao umewaongoza kwenye uraibu mkubwa. Hata hivyo, hatuwasaidii walevi kwa kuwasameheme au kuhalalisha uraibu wao. Yesu alisema hatuwezi kutumikia mabwana wawili (Luka 16:13). Hata ingawa muktadha wa kauli yake ni fedha, kanuni hiyo hiyo inatumika kwa kitu chochote kinachotutawala sisi isipokuwa Mungu. Ni lazima tufanye yote tuwezayo ili kuwasaidia watu watoke kwenye ngome yoyote ya dhambi inayowafunga ili waweze kumtumikia na kumwabudu Mungu kwa moyo wao wote.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je! Wakristo wanapaswa kuwatizama waraibu wa pombe namna gani? Je! Biblia inasema nini kuhusu walevi?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries