settings icon
share icon
Swali

Je! Ninawezaje kufikia ushindi katika Yesu?

Jibu


Kama wafuasi wa Yesu Kristo, sisi wote tunataka kuishi maisha ya Ukristo yenye ushindi. Biblia inatuhakikishia kwamba Mungu na Mwanawe Yesu ni Washindi na kwamba waumini wanaweza kushiriki katika ushindi wao: “Lakini ashukuriwe Mungu, yeye atupaye ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo” (1 Wakorintho 15:57). Kwa namna ya vitendo, tunawezaje kuishi maisha ya ushindi ambayo yamewezekana katika Kristo? Je! tunawezaje kufikia ushindi katika Yesu?

Hatimaye ushindi ni wa Bwana Mungu wetu (1 Samueli 17:47). Tangu siku za Kutoka kwa Israeli kule Misri, wakati wowote watu wa Mungu walimtegemea Yeye pekee, Aliwapa ushindi juu ya adui wao (Kutoka 15). Manabii wa Agano la Kale mara kwa mara walizungumzia kuhusu Mwokozi atakayekuja ambaye ataleta ushindi kamili wa Mungu: “Shangilia sana, ee Binti Sayuni! Piga kelele, Binti Yerusalemu! Tazama, Mfalme wako anakuja kwako, ni mwenye haki, naye ana wokovu, ni mpole, naye amepanda punda, mwana-punda, mtoto wa punda” (Zekaria 9:9; soma pia Zaburi 110:1). Tunajua unabii huu unamrejelea Yesu Kristo, Masihi aliyeahidiwa, ambaye ameushinda ulimwengu (Yohana 16:33).

Yesu alishinda ushindi mkuu pale msalabani. Dhambi ilipatanishwa, na nguvu ya dhambi na mauti ilivunjwa (ona Yohana 12:31 na Petro 2:24). Baada kusulubiswa na kuzikwa kwa Kristo, alifufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu baadaye, na sasa tunashiriki ushindi huo. Shetani alifikiri alikuwa ameshinda shindano kuu kupitia kifo cha Kristo. Badala yake, kifo hicho kilifungua minyororo yetu, kikatuweka huru kutoka katika gereza la dhambi, na kunyang’anya nguvu za giza uwezo: “Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote, akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake. Mungu akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuziburura kwa ujasiri, akizishinda katika msalaba wa Kristo.” (Wakolosai 2:13-15).

Ufunguo wa kupata ushindi katika Yesu ni imani katika Kristo: “Kwa maana kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, yaani, hiyo imani yetu. Ni nani yule aushindaye ulimwengu? Ni yule tu aaminiye kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu” (1 Yohana 5:4-5; pia soma Warumi 8:37). Hatua ya kwanza kwa ushindi katika Yesu ni kumkubali Kristo kama Mwokozi. Tunampokea Bwana kwa neema kwa njia ya imani, na tunaishi katika ushindi wake kwa neema kupitia imani pia. Wokovu wetu ni zawadi kutoka kwa neema ya Mungu, na ushindi katika Yesu ni zawadi ya Mungu ya neema (Waefeso 2:4-8; Wagalatia 3:3).

Je! ni kiwango gani cha ushindi wa Yesu Kristo unachotupatia? Ushindi ambao Yesu anashiriki nasi ni pamoja na ushindi dhidi ya tamaa ya mwili, tamaa ya macho, na kiburi cha uzima (1 Yohana 2:16). Ushidi wa Bwana wetu juu ya majaribu na dhambi (Waebrania 4:15; pia soma Mathayo 4:1-11) umekuwa ushindi wetu vivlevile: “Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake” (Wagalatia 5:24; pia soma Warumi 5:20-21). Mtume Yohana aeleza hivi: “Lakini mwajua ya kuwa yeye alidhihirishwa ili aziondoe dhambi, wala ndani yake hamna dhambi. Kila mtu akaaye ndani yake hatendi dhambi. Kila mtu atendaye dhambi hakumwona yeye wala hakumtambua. Watoto wapendwa, mtu yeyote asiwadanganye. Kila mtu atendaye haki ana haki, kama yeye alivyo na haki. Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi” (1 Yohana 3:5-8).

Yesu amemshinda Shetani na nguvu za giza (Yohana 14:30; 16:11; Marko 1:23-27; Luka 4:33-36, na Anashiriki ushindi huo pamoja nasi. Yesu anasema, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme wa radi. Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru” (Luka 10:18-19 pia soma Waefeso 1:21-22). Mwandishi wa Waebrania anaelezea kuwa Yesu alitwaa mwili na damu na kushiriki katika ubinadamu wetu “ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani ibilisi, na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti” (Waebrania 2:14-15). Hatufai kuogopa kifo wala shetani kwa sababu tunashiriki katika Kristo ushindi juu yao (Matendo 2:24; Warumi 6:9; 8:38-39; 2 Timotheo 1:10; Ufunuo 1:18).

Maadamu tunapokuwa katika ulimwengu huu ulioanguka, bado tatakuwa na mapambano ya kushinda na vita vya kupigana. Wakati mwingine tutaanguka na kushindwa. Lakini tunaendelea kuinuka, tukimwomba Mungu atupatie neema na uwezo wake wa kushinda (2 Wakorintho 12:9). Kama waumini, tunapigana vita vyetu katika ulimwengu wa kiroho, kwa magoti yetu: “Ingawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo. Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome” (2 Wakorintho 10:3-4). Mungu ametupatia silaha ya kiroho ya kutulinda kutokana na nguvu za giza ambazo hutupiga vita (Waefeso 6:10-20).

Ushindi katika Yesu ni kweli na unaweza kufikiwa kwa sababu Bwana Yesu amemshinda Shetani na kila nguvu za giza za ulimwnegu. Tunafikia ushindi katika Yesu kwa kupumzika katika Kristo (Mathayo 11:28) na kumtegemea kutushindania (Warumi 5:17). Bado tungali katika ulimwengu, Bwana anatawala kwa ushindi kupitia kwa wale ambao wamekombolewa kutoka kwa ufalme wa giza na kubadilishwa hadi uflame Wake wa utukufu na nuru (1 Petro 2:9). Hata hivyo, siku itakuja ambapo ushindi wa Yesu utatimizwa kikamilifu na kusherehekewa katika mbingu na dunia mpya: “Yeye atameza mauti milele. Bwana Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote; ataondoa aibu ya watu wake duniani kote. Bwana amesema hili” (Isaya 25:8).

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je! Ninawezaje kufikia ushindi katika Yesu?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries