settings icon
share icon
Swali

Ni njia ipi sahihi ya kupambana na dhambi maishani mwangu?

Jibu


Njia mwafaka ya kushughulikia dhambi ni kuiungama kwa Mungu na kuiacha. Kila moja ya hatua hizi mbili za msingi zinastahili kuangaliwa kwa karibu:

Kwanza, kuungama ndio njia sahihi ya kushughulikia dhambi. Kwa kawaida, ili kiuungama dhambi zetu, ni lazima tutambue kwamba kile ambacho tumefanya (au ambacho hakijafanywa) ni dhambi. Kila mtu amefanya dhambi, na wanaomwamini Kristo pia wanatenda dhambi. Mtume Yohana, akiwaandikia waumini, alisema, “Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu.” (1 Yohana 1:8).

“Kukiri” ni “kukubaliana.” Ili kushughulikia dhambi ipasavyo maishani mwetu, ni lazima tukubaliane na Mungu kuhusu tabia zetu; ikiwa Biblia inaita kitu ambacho tumekuwa tukifanya ”dhambi,” basi tunapaswa kukiita ”dhambi” pia. Katika kukiri kwetu, tunapaswa kuwa na ujasiri wa kutosha kuwa waaminifu kabisa mbele za Bwana. Tunapaswa kuanza kwa kuungama dhambi zote zinazojulikana na kisha kumwomba Bwana afunue dhambi nyingine yoyote ambayo inaweza hitaji kuungamwa.

Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu, nijaribu na ujue mawazo yangu. Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu, uniongoze katika njia ya milele” (Zaburi 139:23-24). Kibiblia Maungamo yetu yanafanywa kwa Mungu, si kwa kuhani. Yesu ndiye Mpatanishi wetu (1 Timotheo 2:5).

Tunapoishughulikia dhambi ipasavyo kwa njia ya kuungama, tuna ahadi hii: “Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote” (1 Yohana 1:9). Ahadi hii ilikuwa ya kutia moyo kwa watu ambao Yohana alikuwa akiwaandikia katika karne ya kwanza Baada ya Kristo (BK), na ni himizo kwetu hii leo. Hiki ndicho kiini cha injili. Yesu ameketi kwenye kiti cha enzi mkono wa kuume wa Mungu Baba, cheo cha nguvu na ushawishi. Yeye huwaombea wale walio wake, waliofanywa hivyo kwa neema na kwa njia ya imani. Wakati mtu aliye ndani ya Kristo anatenda dhambi, ni kana kwamba Yesu anamwambia Baba yake, “Nimeshalipia dhambi hiyo.” Naye Baba anatusamehe kwa msingi wa dhabihu ya Yesu msalabani. Yeye ni mwaminifu kufanya hivyo, kwa kuzingatia ahadi yake; na Yeye ana haki ya kufanya hivyo tu, kwa sababu Yesu amekwisha lipia gharama ya dhambi.

Pili, kuacha dambi ndio njia sahihi ya kushughulikia dhambi. Yesu alipomsamehe mwanamke aliyepatikana katika uzinzi, alimwambia, “kuanzia sasa usitende dhambi tena” (Yohana 8:11). Nenda-hili ni neno la msamaha na kuachiliwa. Usitende dhambi tena-hilo ni agizo la Mungu la kuishi maisha matakatifu.

Hatuwezi kudai kuwa tunaishughulikia dhambi kwa dhati ipasavyo ikiwa tunakataa kuiacha. Ikiwa tunapata nyoka mwenye sumu kali ndani ya nyumba, hatuchezi naye; tunamwondoa kwenye jengo. Tukigundua saratani katika mwili wetu, hatufanyi shughuli zetu kama kawaida; tunaanza mpango mkali wa matibabu ili kupata afya njema. Na ikiwa tunatambua dhambi katika maisha yetu, tunafanya yote tuwezayo kubadili tabia zetu ili kumpendeza Bwana.

Ili kushughulikia dhambi ipasavyo, hatupaswi tu kuiacha dhambi hiyo bali kutafuta pia ukombozi kwa makossa yetu inapowezekana. Zakayo ni mfano mzuri wa hili (Luka 19:8). Tunapaswa kuchukua hatua ili tuepuke kuanguka katika mtego huo tena. Hii ina maana ya kuanzisha tabia mpya, kutembelea sehemu mbalimbali mara kwa mara, na kuepuka watu fulani: “Mtu mwenye marafiki wengi wanaweza kumharibu, bali yuko rafiki aambatanaye na mtu kwa karibu kuliko ndugu” (Mithali 18:24). Tunapaswa kutii amri ya Mungu: “Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi” (Waefeso 6:11).

Ili kushughulikia dhambi ipasavyo, ni lazima tufuate maagizo katika Neno la Mungu. Ni lazima “Tukeshe na kuomba, tusije tukaingia majaribuni” (Marko 14:38). Na lazima tuwe makini kwa uongozi wa Roho Mtakatifu. Wakati Roho amehuzunishwa, ni wakati wa kuungama dhambi zetu na kuziacha (ona Waefeso 4:30).

Wakati tunaishughulikia dhambi ipasavyo maishani mwetu, maisha yetu yatabadilika, na “kuzaa matunda yastahiliyi toba ” (Luka 3:8). Tutaishi kwa ujasiri kwamba dhambi zetu, zilizopita, za sasa na zijazo, zimesamehewa katika Kristo (Warumi 8:1). Tutamsifu Bwana wa wokovu wetu kama Yule anayeweza kutuzuia tusijikwae (Yuda 1:24-25). Tutamwamini akamilishe ndani yetu kazi aliyoianza (Wafilipi 1:6).

Tunaposhughulikia dhambi ipasavyo maishani mwetu, tutathibitisha ukweli wa Mithali 28:13: “Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.” (msisitizo umeongezwa).

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Ni njia ipi sahihi ya kupambana na dhambi maishani mwangu?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries