settings icon
share icon
Swali

Je! Majaribu ni dhambi? Je! ni dhambi kujaribiwa ?

Jibu


Majaribu, kwa asili yake yenyewe huhisi vibaya. Sheria ya maadili ya Mungu imeandikwa katika moyo wa kila mwanadamu (Warumi 1:20), na jaribu la dhambi linapoletwa, dhamiri zetu huhisi hatari mara moja. hata hivyo, jaribu lenyewe si dhambi. Yesu alijaribiwa (Marko 1:13; Luka 4:1-13), lakini hakutenda dhambi kamwe (Waebrania 4:15). Dhambi hutokea wakati tunapoyashughulikia majaribu vibaya.

Tunajaribiwa kupitia njia mbili: Shetani na mwili wetu wenye dhambi. Matendo 5 inatoa mfano wa mtu aliyejaribiwa na Shetani. Anania na mkewe, Safira, wakitaka waonekane wa kiroho zaidi kuliko walivyokuwa kikweli, waliwadanganya mitume na kujifanya walikuwa wanatoa bei kamili ya mali waliyouza. Petro aliwakabili: “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja?” (aya ya 3). Katika kisa hiki, Petro alijua kwamba kishawishi cha kusema uongo kilitoka kwa Shetani. Anania na mkewe wote walikubali jaribio hilo (mistari ya 7-10). Kusalitiwa kwa Yesu na Yuda Iskariote pia kunahusishwa na ushawishi wa Shetani (Luka 22:3; Yohana 13:2).

Hatimaye, kwa kuwa Shetani ndiye “mungu wa ulimwengu huu” (2 Wakorintho 4:4) na baba wa uongo (Yohana 8:44), uovu wote hutoka kwake. Hata hivyo, ubinafsi wetu wenyewe ni mshirika wa Shetani. Hatuhitaji kuchochewa na Shetani ili kuwa na mawazo yenye dhambi. Yakobo 1:13-14 inasema, “Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu yeyote. Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya.”

Ingawa tunaweza kutamani kufanya mema, sote tunajaribiwa. Hakuna aliye juu ya mambo yote, hata mtu na kama mtume Paulo. Alishiriki pambano lake mwenyewe la mwili dhidi ya roho alipoandika katika Warumi 7:22-23, “Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia sheria ya Mungu. Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu.”

Majaribu yenyewe si dhambi. Yanakuwa dhambi wakati tunayaruhusu majaribu kuwa tendo, hata katika akili zetu. Tamaa, kwa mfano, ni dhabi hata ingawa haijatendwa (Mathayo 5:28). Tamaa, kiburi, uchoyo, na husuda zote ni dhambi za moyo; ingawa hazionekani na mtu mwingine, bado nidhambi (Warumi 1:29; Marko 7:21-22). Tunapojiingiza katika jaribu la kuwa na mawazo kama hayo, hutia mizizi ndani ya mioyo yetu na kututia unajisi (Mathayo 15:18-19). Tunapokubali majaribu, tunabadilisha tunda la Roho na tunda la mwili (Waefeso 5:9; Wagalatia 5:19-23). Na mara nyingi, kile kilichokubaliwa kwanza kama wazo kinakuwa kitendo (soma Yakobo 1:15).

Kinga bora dhidi ya kutumbukia katika majaribu ni kuyakimbia katika pendekezo la kwanza. Yusufu ni mfano mkuu wa mtu ambaye hakuruhusu majaribu kuwa dhambi (Mwanzo 39:6-12). Ingawa alijaribiwa kufanya dhambi ya ngono, hakulipa jaribio nafasi kufanyika. Alitumia miguu ambayo Mungu alimpa na kukimbia. Badala ya kukaa katika hali inayoweza kuwa hatari na kujaribu kuzungumza, kutoa sababu, kutetea, kueleza, au kudhoofisha azimio lake, Yusufu alitoroka. Jaribio halikuwa dhambi kwake kwa sababu alipigana nalo kwa njia inayomheshimu Mungu. Ingeweza kuwa dhambi kwa urahisi sana ikiwa Yusufu angekaa karibu nalo na kujaribu kushinda jaribio kwa nguvu zake mwenyewe.

Warumi 13:13-14 inatupa mwongozo wa kuepuka hali zinazoweza kutuongoza kwenye majaribu. “Basi na tuenende kwa adabu kama inavyopasa wakati wa mchana, si kwa kufanya karamu za ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali jivikeni Bwana Yesu Kristo, wala msifikiri jinsi mtakavyotimiza tamaa za miili yenu yenye asili ya dhambi.” Ikiwa tutaazimia “kutouwezesha mwili kufanya dhambi,” basi tutajikinga sisi wenyewe mbali na hali ambazo huenda zikatujaribu sana. Tunapojiweka katika hali ambayo tunajua kwamba tutajaribiwa, tunajitakia shida. Mungu anaahidi kutoa “njia ya kuponyoka” tunapojaribiwa (1 Wakorintho 10:13), lakini mara nyingi njia hiyo ni kuepuka hali yote kabisa. “Zikimbie tamaa mbaya za ujana” (2 Timotheo 2:22). Yesu alitufundisha kuomba, “Usitutie majaribuni” (Luka 11:4), lakini tuna wajibu wa kuzingatia njia ambayo Mungu anatuongoza na kuepuka majaribu wakati wowote tunapoweza.

EnglishRudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je! Majaribu ni dhambi? Je! ni dhambi kujaribiwa ?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries