settings icon
share icon
Swali

Kufuru ni nini? Je, matumizi mabaya ya kitu kilicho wakfu inamaanisha nini?

Jibu


Kufuru ni matumizi mabaya ya mtu, mahali au kitu kitakatifu. Kufuru hutokea pale mtu anapotumia vibaya kitu kitakatifu, kukashifu mahali patakatifu, au kuzungumza kwa njia isiyo ya heshima kuhusu kitu chochote kinachohusiana na Mungu au dini. Neno hili lina asili ya Kilatini: sacer (“takatifu”) na legere (“kuiba”). Hapo mwanzo neno kufuru huenda lilirejelea vitendo vya wanyang’anyi wa makaburi walioharibu makaburi lakini sasa linarejelea “kuiba” kwa utakatifu wowote kutoka mahali, kitu au mtu wa kidini.

Mfalme Belshaza wa Babeli alitenda dhambi ya kukufuru katika karamu alipotoa “amri ya kuleta vile vikombe vya dhahabu ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka Hekalu la Mungu huko Yerusalemu, naye mfalme na wakuu wake, wake zake na masuria wake wakavinywea.Walipokuwa wakinywa mvinyo, wakaisifu miungu ya dhahabu na fedha, ya shaba, chuma, miti na mawe.” (Danieli 5:3–4). Hii ilikuwa mojawapo ya matendo ya mwisho ya Belshaza, kwani aliuawa usiku huohuo (mstari wa 30).

Nadabu na Abihu, wana wawili wa Haruni, walitenda dhambi ya kukufuru walipotoa “moto usio halali mbele za Bwana, kinyume na agizo ya Mungu” (Mambo ya Walawi 10:1). Matumizi mabaya ya ofisi yao takatifu yalisababisha msiba: “moto ukaja kutoka kwa uwepo wa Bwana na kuwaramba, nao wakafa mbele za Bwana.” (mstari wa 2). Bila shaka, Mungu huzingatia dhambi ya kukufuru kuwa kosa kubwa.

Hema (na, baadaye, hekalu) katika Agano la Kale ilikuwa mahali ambapo Mungu angekutana na watu Wake. Jengo na kila kitu kilicho ndani yake—kama vile sanduku la agano—lilinyunyiziwa damu ya dhabihu takatifu na kwa hivyo kutengwa kwa ajili ya Mungu. Ni makuhani tu, ambao pia walitakaswa kwa Bwana kwa ajili ya huduma, ndio waliruhusiwa kuingia kwenye hema. Mungu alimuua yeyote aliyekiuka hema au kukufuru vyombo vitakatifu (Hesabu 16:1–40; 2 Samweli 6:6–7). Patakatifu pa Patakatifu palitengwa kutoka kwa sehemu nyingine ya hema kwa pazia nene na kuhani mkuu angeweza kuingia mara moja tu kwa mwaka wakati alipotoa dhabihu ya damu kwa ajili ya dhambi za watu. Somo moja ambalo hema ilifundisha ni kwamba Mungu ni mtakatifu na sisi sio watakatifu—na hatuthubutu kumkufuru.

Yesu aliwaonya Mafarisayo dhidi ya mazoea yao ya kukufuru ya kiapo kisicho halali. Katika viapo vyao, Mafarisayo walijaribu kutofautisha kati ya hekalu na dhahabu katika hazina ya hekalu (la mwisho ilikuwa takatifu zaidi machoni pao) na kati ya madhabahu na zawadi kwenye madhabahu (ya mwisho ilikuwa takatifu zaidi machoni pao). Yesu alifundisha kwamba hekalu na kila kitu kilichohusishwa nalo hatimaye kiliwekwa wakfu kwa Mungu, kwa hivyo kiapo chochote kilichofanywa katika sehemu yoyote ya hekalu kilikuwa cha makubaliano ya kubana mbele za Mungu (Mathayo 23:16–22).

Mojawapo ya aina ya kawaida ya kufuru leo ni kukufuru jina takatifu la Mungu na jina la Bwana wetu Yesu. Hii inakiuka Kutoka 20:7, “Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako, kwa kuwa Bwana hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.” (linganisha Zaburi 139:20). Agano Jipya linakataza “maneno mabaya” (Waefeso 4:29), ambayo hakika yanajumuisha kulitumia jina la Mungu kama neno la kiapo.

Ingawa makanisa mengine leo yana watakatifu na vitu “vitakatifu”, hakuna sababu ya kibiblia ya kuinua mtu mmoja, mahali, au kitu kama “kitakatifu” zaidi kuliko kingine. Waumini wote, si wachache waliochaguliwa tu, “mnajengwa kuwa nyumba ya kiroho, ili mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo” (1 Petro 2:5). Hekalu la Agano la Kale limetoweka, na sasa sisi ni “jengo la Mungu” (1 Wakorintho 3:9). Paulo anawauliza waumini, “ Je, hamjui ya kwamba ninyi wenyewe ni hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?” (mstari wa 16). Ikiwa mtu leo ataandika maneno ya kufuru upande wa jengo la kanisa, kwa kweli ni tendo la kufuru, lakini si kwa sababu mbao na mawe ya jengo hilo ni vitakatifu. Nia ya mwenye kufuru ni kumdharau Mungu, na katika akili yake analenga tendo lake kwa uwakilishi unaopatikana na dhahiri wa Mungu. Nia hiyo ndiyo inayofanya uharibifu huo kuwa wa kufuru, na Mungu hutazama moyo.

Hata mifumo ya kidini inaweza kukuza kufuru, ikiwa “wataiba” utakatifu wa Mungu na kuutumia kwa watu au vitu. Makanisa yanayotakasa wahusika wa biblia au watu mashuhuri wa kihistoria, kuomba kwa watakatifu, kuamuru ibada ya sanamu au masalia, au kukuza heshima kwa vitu vya kimwili yana hatia ya kufuru. Watu ambao Mungu amewatumia wanapaswa kuonyeshwa heshima na kujifunza kutoka kwao, lakini bado ni watenda dhambi waliookolewa kwa neema. Vitu vya kimwili vinaweza kuwa na umuhimu wa kihistoria au maana kama ishara za kidini, lakini havipaswi kupigigwa magoti , kuomba kwao, au kutafutwa kama njia ya kupata neema.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Kufuru ni nini? Je, matumizi mabaya ya kitu kilicho wakfu inamaanisha nini?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries