settings icon
share icon
Swali

Je, ni kanuni gani za kibiblia za kufanya uamuzi thabiti?

Jibu


Maamuzi thabiti yanaanza kwa kutambua mapenzi ya Mungu. Mungu hufurahi katika kufunua mapenzi Yake kwa wale wanaotamani kufuata maagizo Yake (Zaburi 33:18, 35:27; 147:11). Mtazamo wetu juu ya kufanya uamuzi unapaswa kuwa ule wa Yesu Mwenyewe ambaye alithibitisha, "Sio mapenzi Yangu, bali yako yatendeke" (Luka 22:42; Mathayo 6:10).

Mungu hufunua mapenzi yake kwetu hasa kwa njia mbili. Kwanza, kupitia Roho Wake: "Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake"(Yohana 16:13; tazama pia 1 Yohana 2:20, 27). Na, pili, Mungu anafunua mapenzi Yake kupitia Neno Lake: "Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu" (Zaburi 119:105, tazama pia Zaburi 19:7-9, 2 Petro 1:19).

Utaratibu wa kufanya maamuzi ni pamoja na kufanya hukumu kuhusu mtazamo au kitendo. Maamuzi ni tendo la mapenzi, na daima huathiriwa na akili, hisia, au zote mbili. Maamuzi tunayofanya kweli yanaonyesha tamaa za moyo wetu (Zaburi 119:30). Kwa hivyo, swali kuu kabla ya kufanya uamuzi ni "Je, ninachagua kujipendeza mwenyewe, au je, ninachagua kumpendeza Bwana?" Yoshua aliweka kiwango: "Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia ... Lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana "(Yoshua 24:15, tazama Warumi 12:2).

Mungu anaona picha nzima-ya zamani, ya sasa, na ya baadaye ya maisha yetu. Anatufundisha na kutushauri vile anajidhihirisha kwetu kupitia Neno Lake na Roho Wake. Mungu ametupatia ahadi hii: "Nitakufudisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; nitakushauri, jicho langu likikutazama"(Zaburi 32:8; tazama Zaburi 25:12). Kutakuwa na wakati ambapo mapenzi ya Mungu inaweza kuonekana kuwa yasiyofaa au yasiyopendeza, wakati moyo wetu utafuata tamaa zetu wenyewe badala ya kumwamini Mungu. Lakini hatimaye tutajifunza kwamba mapenzi ya Mungu daima ni kwa manufaa yetu (Zaburi 119:67; Waebrania 12:10-11).

Tena, msingi mkuu wa kufanya maamuzi thabiti ni kujua mapenzi ya Mungu na si kufuata tamaa za mioyo yetu wenyewe: "Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, lakini mwisho wake ni njia za mauti" (Mithali 14:12). tazama Methali 12:15; 21:2). Tunapoweka tumaini letu kwa Mungu, badala ya sisi wenyewe, hivi karibuni tunatambua ni maamuzi gani yanayompendeza.

Kwanza, Mungu hubariki maamuzi hayo ambayo Yeye huanzisha na ambayo yanalingana na Neno Lake: "Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu"(Methali 4:11; ona pia Zaburi 119:33). Pili, Mungu hubariki maamuzi ambayo yanatimiza kusudi Lake na kutegemea nguvu Zake: "Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema" (Wafilipi 2:13; tazama pia Wafilipi 4:13).

Zaidi ya hayo, Mungu hubariki maamuzi hayo ambayo yanatokea katika utukufu Wake: "Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lolote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu" (1 Wakorintho 10:31). Anabariki maamuzi ambayo yanaonyesha tabia Yake, ambayo yanakuza haki, wema na unyenyekevu: "Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!"(Mika 6:8; tazama pia 1 Wakorintho 10:31; 1 Timotheo 4:12). Na anabariki maamuzi hayo ambayo yanatoka kwa imani: "Lakini pasipo Imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao" (Waebrania 11:6).

Hatupaswi kusahau ahadi ya Mungu ya kuwapa watoto Wake hekima wakati watauliza: "Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa" (Yakobo 1:5). ; tazama 1 Wathesalonike 5:17). Na wakati tunaombea hekima, tunapaswa kutumaini Mungu kujibu maombi yetu: "Ila na aombe kwa Imani, pasipo shaka yoyote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana"(Yakobo 1:6-7). Uvumilivu ni muhimu, pia, tunapongojea muda wa Mungu: "Baada ya kusubiri kwa uvumilivu, Abrahamu alipokea ile ahadi" (Waebrania 6:15).

Kufanya maamuzi ni ngumu zaidi wakati inahusisha chaguo la chungu. Wakati mwingine, njia sahihi ya kitendo pia itatuumiza kwa namna fulani. Hapa ndipo tunahitaji neema zaidi. Je! Tuko tayari kuteseka kwa ajili ya utukufu wa Kristo? "Basi kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni silaha ya nia ile ile; kwa maana yeye aliyeteswa katika mwili ameachana na dhambi. Tangu sasa msiendelee kuishi katika taama za mwanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani"(1 Petro 4:1-2).

Kufanya uamuzi leo? Angalia Neno la Mungu kwa uongozi. Furahia faraja katika amani ambayo Yeye tu anaweza kutoa (Wafilipi 4:7). Uuliza hekima, tumaini ahadi Zake, na ataongoza njia yako: "Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe. Katika njia zako zote mkiri Yeye, naye atayanyosha mapito yako"(Methali 3:5-6; tazama pia Isaya 58:11; Yohana 8:12).

EnglishRudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je, ni kanuni gani za kibiblia za kufanya uamuzi thabiti?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries