settings icon
share icon

Kitabu cha Ayubu

Mwandishi: Kitabu cha Ayubu hakimtaji bayana mtunzi wake. Watu ambao huenda walikiandika ni Ayubu, Elihu, Musa na Sulemani.

Tarehe ya kuandikwa: Tarehe ya uandishi wa kitabu cha Ayubu itajulikana kulingana na mwandishi wa kitabu cha Ayubu. Ikiwa Musa alikuwa mwandishi, tarehe itakuwa karibu 1440 BC. Ikiwa Sulemani alikuwa mwandishi, tarehe itakuwa karibu 950 BC. Kwa sababu hatumjui mwandishi, hatuwezi kujua tarehe ya kuandika.

Kusudi la Kuandika: Kitabu cha Ayubu kinatusaidia kuelewa yafuatayo: Shetani hawezi kuleta uharibifu wa kifedha na kimwili juu yetu isipokuwa ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Mungu ana nguvu juu ya kile Shetani anaweza kufanya na kile ambacho hawezi kufanya. Ni zaidi ya uwezo wetu wa kibinadamu kuelewa "ni sababu gani" iliyo nyuma ya mateso yote duniani. Waovu watapata haki wanazostahili. Hatuwezi kamwe kulaumu mateso yetu na dhambi juu ya maisha yetu. Mateso wakati mwingine yanaweza kuruhusiwa katika maisha yetu ili kusafisha/kutakasa, kujaribu, kufundisha au kuimarisha roho. Mungu bado anatosha, anastahili na anaomba upendo wetu na sifa katika hali zote za maisha.

Mistari muhimu: Ayubu 1: 1, "Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu.."

Ayubu 1:21, " akasema, mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe"

Ayubu 38: 1-2, "Ndipo Bwana akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, 'Ni nani huyu atiaye mashauri giza kwa maneno yasiyo na maarifa?'"

Ayubu 42: 5-6, "Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona. Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu katika mavumbi na majivu.".

Muhtasari kwa kifupi: Kitabu kinaanza kwa mandhari mbinguni ambapo Shetani anakuja kumshtaki Ayubu mbele za Mungu. Anasisitiza kwamba Ayubu anamtumikia Mungu kwa sababu Mungu anamlinda na anataka idhini ya Mwenyezi Mungu ili ajaribu imani na uaminifu wa Ayubu. Mungu anampa idhini yake, tu kwa mipaka fulani. Ni kwa nini wenye haki wanateseka? Hili ndilo swali linaloulizwa baada ya Ayubu kupoteza familia yake, mali yake, na afya yake. Marafiki watatu wa Ayubu Elifazi, Bildadi, na Sofari, wanakuja kumpoza na kujadili mfululizo wa majanga yanayomkumba. Wanasisitiza kwamba mateso yake ni adhabu kwa ajili ya dhambi katika maisha yake. Ayubu, ingawa, bado anajitolea kwa Mungu kwa haya yote na anashikilia kauli kuwa maisha yake hajawahi kuwa ya dhambi. Mtu wa nne, Elihu, anamwambia Ayubu kuwa anahitaji kujinyenyekeza na ajisalimishe kwa matumizi ya Mungu ya majaribio kwa kutakasa maisha yake. Hatimaye, Ayubu anamuuliza Mungu mwenyewe na kujifunza mafunzo muhimu kuhusu mamlaka ya Mungu na haja yake kwa kumuamini Bwana hakika. Kisha Ayubu anarejeshwa kwa afya nzuri, furaha na mafanikio zaidi ya hali yake ya awali.

Ishara: Ayubu alipokuwa akiwaza chanzo cha masaibu yake, maswali matatu yakamjia akilini mwake, ambayo yote yamejibiwa tu katika Bwana wetu Yesu Kristo. Maswali haya yanatokea katika sura 14. Kwanza, katika mstari wa 4, Ayubu anauliza "Nani anaweza kuleta kile ambacho ni safi kutoka kwa kisichokuwa safi? Hakuna mtu !?" Swali la Ayubu linatoka kwa moyo ambao unatambua kuwa hauwezi kumpendeza Mungu au uwezi kuhesabiwa haki mbele zake. Mungu ni mtakatifu; ila sisi si watakatifu. Kwa hivyo kuna shimo kubwa/ghuba baina ya mwanadamu na Mungu, iliyosababishwa na dhambi. Lakini jibu kwa swali la machungu la Ayubu linapatikana katika Yesu Kristo. Amelipa deni kwa ajili ya dhambi zetu na badala yake amezibadilisha kwa haki yake, na hivyo kutufanya kukubalika mbele za Mungu (Waebrania 10:14; Wakolosai 1: 21-23; 2 Wakorintho 5:17).

Swali la pili la Ayubu, "" Lakini mtu anakufa na kulala kifudifudi; Mtu anazeeka/anaisha, na ako wapi yeye? " (Vs. 14) ni swali lingine kuhusu uzima wa milele na kifo ambalo limejibiwa tu katika Kristo. Pamoja na Kristo, jibu kwa 'ako wapi yeye?' Ni uzima wa milele mbinguni. Bila Kristo, jibu ni katika "giza la nje" milele ambapo kuna "kulia na kusaga meno" (Mathayo 25:30).

Swali la Ayubu la tatu, linalopatikana katika mstari wa 14, ni "Ikiwa mtu atakufa, ataishi tena?" Kwa mara nyingine tena, jibu linapatikana katika Kristo. Hakika tutaishi tena ikiwa tumo ndani yake Kristo. ".Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, mauti imemezwa kwa kushinda. Ku wapi, ewe mauti, uchungu wako'"(1 Wakorintho 15: 54-55).

Vitendo tekelezi: Kitabu cha Ayubu kinatukumbusha kwamba kuna "vita vya ulimwengu mzima" vinavyoendelea nyuma ya mandhari ambavyo kawaida hatujui chochote kuvihusu. Mara nyingi tunashangaa ni kwa nini Mungu anaruhusu kitu, na tunaulizia au tunatia shaka wema wa Mungu, bila kuona picha kamili. Kitabu cha Ayubu kinatufundisha kumwamini Mungu katika hali zote. Lazima tumwamini Mungu, sio tu WAKATI hatuelewi, bali kwa SABABU hatuelewi. Zaburi inatuambia " Mungu, njia yake ni kamilifu" (Zaburi 18:30). Ikiwa njia za Mungu ni "kamilifu," basi tunaweza kuamini kwamba lolote afanyalo-na lolote analoruhusu-pia ni kamilifu. Hili haliwezekani kwetu, lakini mawazo yetu si mawazo ya Mungu. Ni kweli kwamba hatuwezi kutarajia kuelewa mawazo yake kikamilifu, kama anavyotukumbusha "Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu, asema Bwana. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu "(Isaya 55: 8-9). Hata hivyo, wajibu wetu kwa Mungu ni kumtii, kumwamini na kujiwasilisha kwa mapenzi yake, iwe tunaelewa au la.

English

Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Kitabu cha Ayubu
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries