settings icon
share icon
Swali

Je, tunapaswa kujifunza nini kutoka kwa maisha ya Isaka?

Jibu


Jina Isaka, ambalo linamaanisha "anacheka," lilitokana na majibu ya wazazi wake wakati Mungu alimwambia Ibrahimu akiwa na umri wa miaka 100, naye mkewe Sarah, akiwa na umri wa miaka 90, kwamba atampata mwana (Mwanzo 17 : 17; 18:12). Isaka alikuwa mwana wa pili wa Abrahamu; mwana wake wa kwanza, Ishmaeli, alikuwa mwana wa mjakazi wa Sara, Hajiri. Hii ilisababishwa na ukosefu wa subira wa Sara katika kumpa Ibrahimu familia (Mwanzo 16: 1-2). Punde tu Isaka alipoachishwa kunyonya, Sara alisisitiza kwamba Ibrahimu amfukuze Hajiri na mwanawe, kuhakikisha kwamba urithi wa familia ungeenda kwa Isaka (Mwanzo 21: 3-12).

Miaka mingi baadaye, Isaka alichukuliwa na baba yake juu ya mlima ambapo Abrahamu, kwa kumtii Mungu, aliandaa kumtoa kama sadaka (Mwanzo 22: 1-14). Abrahamu, Isaka, na watumishi wawili wa Abrahamu walipanda punda na wakaanza safari ya siku tatu kwenda Mlima Moriya. Abrahamu aliwaacha watumishi wake nyuma, na pamoja na Isaka walichukua mbao, kisu, na vifaa vya moto, huku wakisema watasali na kisha kurudi. Isaka aliuliza juu ya mahali alipokuwa yule kondoo kwa ajili ya sadaka. Abrahamu akamwambia Isaka kwamba Mungu Mwenyewe angeweza kumtoa mwana-kondoo. Abrahamu alijenga madhabahu na kumfunga Isaka juu yake. Biblia haijasema ikiwa Isaka alipinga ama hakupinga. Abrahamu alipojiandaa kumwua Isaka, malaika alisimamisha shughuli hiyo. Abrahamu kisha aliona kondoo mume aliyenaswa pembe zake katika kichaka na akamtoa awe sadaka. Huu ni mfano wa kuvutia ambao unalinganishwa na Mungu alipotoa mwanawe peke yake, Yesu, kuwa dhabihu. Mungu, kwa kweli alitoa Mwana-Kondoo-halisi kwa ajili ya Ibrahimu na Isaka kisha na kwa mfano, kwa binadamu wanaokubali dhabihu ya Yesu (Yohana 1:29; Waebrania 10).

Sara alikufa wakati Isaka alikuwa takribani miaka thelathini na, akielekea arobaini. Baada ya kifo chake, Abrahamu alimtuma mmoja wa watumishi wake ili kumtafutia Isaka mke kutoka kwa jamaa zao, kwa kuwa Abrahamu aliamua kuwa mwanawe hatamwoa Mkanaani (Mwanzo 24: 1-51). Mtumishi wa Abrahamu aliomba ili kufanikiwa katika kutafuta mke mzuri, na Mungu aliamuru jitihada zake. Alipokuwa na miaka arobaini, Isaka alioa binamu yake Rebeka (Mwanzo 25:20). Biblia inatuambia kwamba "alimpenda, na Isaka alifarijika baada ya kifo cha mama yake" (Mwanzo 24:67).

Isaka alipokuwa na miaka sitini, alijaliwa mapacha-Yakobo na Esau. Isaka alipendelea Esau, mwanawe wa kwanza naye Rebeka alipendelea Yakobo. Hii ilisababisha ushindani mkubwa ndani ya familia na kusababisha Yakobo, mwana mdogo, kupokea urithi na baraka ya baba yake ambayo ingekuwa yake Esau, mwana wa kwanza. Hii ni baada ya Isaka na Esau walipopotoshwa na Rebeka na Yakobo. Isaka alipata kujua kuhusu udanganyifu huo lakini hakuweza kuondoa ile baraka kutoka kwa Yakobo (Mwanzo 27). Rebeka alipata kujua mpango wa Esau wa kumwua Yakobo baada ya kifo cha Isaka na kumshawishi Isaka kumtuma Yakobo kwa nduguye Labani ili kutafuta mke kati ya jamaa zake. Isaka tena alimbariki Yakobo kabla ya kumtuma, akisali kwamba Mungu atampa Yakobo baraka iliyotolewa kwa Abrahamu.

Abrahamu alikufa wakati Isaka alipokuwa na takribani miaka sabini na tano na kumwachia kila kitu alichokuwa nacho (Mwanzo 25: 5). Ingawa Ishmaeli alikuwa amefukuzwa wakati Isaka alipoachishwa kuunyonya, Isaka na Ishmaeli walimzika Abrahamu (Mwanzo 25: 9). Biblia haijazungumzia hasa uhusiano wao wawili. Wazao wa Ishmaeli na wa Isaka wamekuwa maadui kwa kihistoria; uadui huo upo mpaka leo. Lakini ni jambo la kupendeza kuona kwamba wanaume hao wawili wanaonekana wameungana kwa kuomboleza baba yao.

Wakati kulipokuwa na njaa katika nchi hiyo, Mungu alimtokea Isaka na kumwambia asiende Misri lakini kubaki katika nchi hiyo. Mungu aliahidi kuwa pamoja na Isaka na kumbariki na kuwapa ardhi wazao wa Isaka. Mungu alithibitisha agano alilolifanya na Abrahamu, akisema kuwa angefanya wazao wake kuwa wengi kama nyota na kubariki mataifa yote ya dunia katika uzao wake (Mwanzo 26: 1-6).

Isaka alibaki katika nchi ya Kanaani. Lakini sawia vile baba yake alivyofanya miaka mingi kabla ya kuzaliwa kwake, kwa kuhofia, Isaka alimwonyesha Rebeka kama dada yake badala ya mkewe (Mwanzo 26: 7-11). Lakini, kama Mungu alivyomlinda Sara, pia alimkinga Rebeka. Mungu alimbariki Isaka kwa mazao mengi na utajiri, hivyo basi Wafilisti wakawa na wivu na kuvifukia visima vya maji ambavyo Ibrahimu alikuwa amechimba. Mfalme wa Wafilisti alimwomba Isaka aende, na Isaka alikubali. Alitoka mahali hapo na kwenda kwingine huku akichimba visima vingine wakati adui zake waligombana naye juu ya maji. Punde si punde mfalme wa Wafilisti alitambua kwamba Isaka alikuwa amebarikiwa na Mungu na akafanya mkataba wa amani kati yao (Mwanzo 26: 26-31).

Isaka alikufa akiwa na umri wa miaka mia na themanini na kuzikwa na wanawe wawili. Mungu alithibitisha agano lake na Yakobo, mwanawe Isaka ambaye alimpa jina la Israeli.

Ijapokuwa hadithi kubwa ya Isaka ni maelezo ambayo hayana masomo mengi tungeweza kuiga katika maisha yetu, katika Isaka tunaona moyo uliojitoa kwa mapenzi ya Mungu. Kwa mfano, alikuwa mtiifu kwa Abrahamu na Sara na anaonekana kuwa na uaminifu kwa mwongozo wao. Alimtii Mungu wakati alimwambia abaki katika nchi licha ya njaa na mashambulizi ya adui zake. Isaka alipogundua kwamba alikuwa amedanganywa na mwanawe Yakobo, alikubali na kusujudia kile alichotambua kama mapenzi ya Mungu, licha ya kuwa kinyume kabisa na utamaduni uliokubaliwa wakati huo. Kama Isaka alivyogundua, sisi pia tunapaswa kukumbuka kwamba njia za Mungu sio kama njia zetu au mawazo yake sio sawa na yetu (Isaya 55: 8). Hadithi ya Isaka pia inaonyesha uaminifu wa Mungu kwa ahadi zake-Alifanya agano na Abrahamu na aliendelea kuimarisha agano hio kwa Isaka na pia kwa Yakobo mwana wa Isaka.

Ingawa hakuna mafanikio makuu ya kuzungumzia juu ya maisha ya Isaka, Mungu alichagua Isaka kuendeleza agano katika uzao wake, uzao ambao ungezalisha Masihi, Yesu. Kwa vizazi vingi, taifa la Kiyahudi lilielezea Mungu wao kama Mungu wa Abrahamu, Isaka, na Yakobo. Hakika, kuna vifungu kadhaa vya Maandiko ambapo Mungu anajielezea Mwenyewe kwa namna ile ile (k.m, Kutoka 3: 6). Isaka ameorodheshwa na mababu wengine wakuu na ana nafasi yake katika ufalme wa Mungu (Luka 13:28). Na hakuna heshima kubwa kuliko hiyo tunayoweza kutumaini kufikia.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je, tunapaswa kujifunza nini kutoka kwa maisha ya Isaka?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries