settings icon
share icon
Swali

Je! Biblia inasema nini kuhusu bikira Maria?

Jibu


Maria mama ya Yesu alielezewa na Mungu kama "mwenye fadhila kuu" (Luka 1:28). Maneno mwenye fadhila kuu hutoka kwa neno moja la Kiyunani, ambalo kimsingi linamaanisha "neema nyingi." Maria alipokea neema ya Mungu.

Neema ni "fadhila isiostahili"; yaani, neema ni baraka tunayopokea licha ya ukweli kwamba hatuistahili. Maria alihitaji neema kutoka kwa Mungu na Mwokozi, kama vile sisi wengine tunavyohitaji. Maria mwenyewe alielewa ukweli huu, kama alivyotangaza katika Luka 1:47, "Roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu."

Bikira Maria, kwa neema ya Mungu, alitambua kwamba alihitaji Mwokozi. Biblia haisemi kamwe kwamba Maria alikuwa yeyote bali mwanadamu wa kawaida ambaye Mungu alichagua kumtumia kwa njia ya ajabu. Ndio, Mariamu alikuwa mwanamke mwenye haki na aliyependwa (neemeshwa) na Mungu (Luka 1:27-28). Wakati huo huo, Maria alikuwa mwanadamu mwenye dhambi ambaye alihitaji Yesu Kristo kama Mwokozi wake, kama vile kila mtu mwingine (Mhubiri 7:20, Warumi 3:23, 6:23; 1 Yohana 1:8).

Bikira Maria hakuwa "mkingiwa dhambi ya asili." Biblia haipendekezi kuzaa kwa Mariamu kulikuwa kitu bali kuzaa wa kawaida wa binadamu. Maria alikuwa bikira wakati alimzaa Yesu (Luka 1:34-38), lakini hakuwa bikira milele. Dhana ya ubikira wa kudumu wa Maria si wa kibiblia. Mathayo 1:25, akizungumza juu ya Yusufu, anasema, "Asimjue kamwe hadi alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake Yesu." Neno hadi linaonyesha wazi kuwa Yusufu na Maria walikuwa na uhusiano wa kawaida wa ngono baada ya kuzaliwa kwa Yesu. Maria alibaki bikira hadi kuzaliwa kwa Mwokozi, lakini baadaye Yusufu na Maria walikuwa na watoto kadhaa pamoja. Yesu alikuwa na kaka wa kambo wanne: Yakobo, Yusufu, Simoni, na Yuda (Mathayo 13:55). Yesu pia alikuwa na dada wa kambo, ingawa hawajatajwa au kuhesabiwa (Mathayo 13:55-56). Mungu alimbariki na kumneemesha Maria kwa kumpa watoto kadhaa, ambayo katika utamaduni huo ilikubalika kama dalili wazi ya baraka za Mungu kwa mwanamke.

Wakati mmoja wakati Yesu alipokuwa akiongea, mwanamke mmoja katika umati alitangaza, "Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya" (Luka 11:27). Hakukuwepo kamwe nafasi nzuri zaidi kwa Yesu kutangaza kwamba Maria alikuwa anastahili sifa na kuabudu. Jibu la Yesu lilikuwa gani? "Afadhali, heri ni walisikiao neno la Mungu na kulishika" (Luka 11:28). Kwa Yesu, kutii Neno la Mungu kulikuwa muhimu zaidi kuliko kuwa mwanamke aliyemzaa Mwokozi.

Hakuna mahali popote katika Maandiko Yesu au mtu yeyote anaelekeza sifa yoyote, utukufu, au kuabudu kwa Maria. Elisabeti, jamaa ya Maria, alimsifu Maria katika Luka 1:42-44, lakini sifa yake ina msingi juu ya baraka ya kuzaa Masihi. Haikuwa na msingi juu ya utukufu wowote wa asili katika Maria. Kwa kweli, baada ya hili Maria alizungumza wimbo wa sifa kwa Bwana, akisifu uzingatifu Wake kwa wale wa hali ya unyenyekevu na rehema na uaminifu Wake (Luka 1:46-55).

Wengi wanaamini kwamba Maria alikuwa ni chanzo cha Luka kuandika Injili yake (angalia Luka 1:1-4). Luka anaandika malaika Gabrieli akimtembelea Maria na kumwambia kwamba angemzaa mwana ambaye angekuwa Mwokozi. Maria hakuwa na uhakika jinsi hili lingeweza kuwa kwa kuwa yeye alikuwa bikira. Wakati Gabrieli alimwambia mwana angezaliwa na Roho Mtakatifu, Maria akajibu, "Mimi ni mtumishi wa Bwana ... Na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akamwacha" (Luka 1:38). Maria alijibu kwa imani na nia ya kujiwasilisha kwa mpango wa Mungu. Sisi pia, tunapaswa kuwa na imani kama hiyo kwa Mungu na kumfuata Yeye kwa uaminifu.

Akielezea matukio ya kuzaliwa kwa Yesu na majibu ya wale ambao walisikia ujumbe wa wachungaji kuhusu Yesu, Luka anaandika, "Lakini Maria akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake" (Luka 2:19). Wakati Yusufu na Maria walimtambulisha Yesu hekaluni, Simeoni alitambua kwamba Yesu alikuwa Mwokozi na akamtukuza Mungu. Yusufu na Maria walishangaa kwa kile Simeoni alisema. Simeoni pia akamwambia Maria, "Tazameni, mtoto huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. (Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako), ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi"(Luka 2:34-35).

Wakati mwingine hekaluni, wakati Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na mbili, Maria alikasirika kwamba Yesu alikuwa amebaki nyuma wakati wazazi Wake walikuwa wameondoka kuenda Nazareti. Walihuzunishwa kumtafuta. Walipompata, bado katika hekalu, Alisema lazima awe katika nyumba ya Baba Yake (Luka 2:49). Yesu alirudi Nazareti pamoja na wazazi wake wa duniani na kuwatii. Tunaambiwa, tena, kwamba Maria "aliyaweka hayo yote moyoni mwake" (Luka 2:51). Kumlea Yesu lazima ilikuwa ni jitihada za kufadhaisha lakini pia kujazwa na wakati wa thamani, labda kumbukumbu ambazo zikawa ni za kutia uchungu zaidi kama Maria alikuja kufahamu vikamilifu zaidi Yesu alikuwa nani. Sisi, pia, tunaweza kuweka moyoni ujuzi wa Mungu na kumbukumbu za shughuli Yake katika maisha yetu.

Alikuwa Maria ambaye alimwomba Yesu kuingilia kati kwenye harusi ya Kana, ambapo alifanya muujiza Wake wa kwanza na akageuza maji kuwa divai. Ingawa Yesu alionekana kumpuuza mwanzoni, Maria aliwaagiza watumishi kufanya kile alichowaambia. Alikuwa na imani Kwake (Yohana 2:1-11).

Baadaye katika huduma ya Yesu ya umma, familia yake ilikua na wasiwasi. Marko 3:20-21 anaandika, "Mkutano wakakusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate. Na jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, 'Amerukwa na akili.'" Wakati familia yake ilipofika, Yesu alitangaza kwamba ni wale ambao wanafanya mapenzi ya Mungu ambao ni familia Yake. Ndugu za Yesu hawakumwamini kabla ya kusulubiwa, lakini angalau wawili wao walimwamini baadaye — Yakobo na Yuda (Yuda), waandishi wa vitabu vya Agano Jipya vyenye majina yao.

Maria alionekana kumwamini Yesu katika maisha Yake yote. Alikuwepo msalabani wakati Yesu alikufa (Yohana 19:25), bila shaka kuhisi "upanga" ambao Simeoni alitabiri ungeingia moyoni mwake. Ilikuwa pale msalabani kwamba Yesu alimwomba Yohana kutumikia kama mwana wa Maria, na Yohana akamchukua Maria nyumbani kwake (Yohana 19:26-27). Maria pia alikuwa pamoja na mitume siku ya Pentekoste (Matendo 1:14). Hata hivyo, Maria hatajwi tena baada ya Matendo sura ya 1.

Mitume hawakumpa Maria jukumu maarufu. Kifo cha Maria hakijaandikwa katika Biblia. Hakuna kinachosemwa kuhusu Maria kupaa mbinguni au kuwa na jukumu la hadhi. Kama mama wa kidunia wa Yesu, Maria anapaswa kuheshimiwa, lakini yeye hastahili ibada yetu au kuabudu kwetu.

Bibilia haionyeshi popote kwamba Maria anaweza kusikia maombi yetu au kwamba anaweza kutupatanisha na Mungu. Yesu ndiye mtetezi na mpatanishi wetu pekee mbinguni (1 Timotheo 2:5). Ikiwa atatolewa ibada, kuabudu, au sala, Maria angeweza kusema sawa na malaika: "Mwabudu Mungu!" (Angalia Ufunuo 19:10; 22:9.) Maria mwenyewe alituwekea mfano, akielekeza ibada yake, kuabuku kwake, na sifa kwa Mungu pekee: "Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; kwa kuwa ameutazama unyonge wa mtumishi Wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa vizazi vyote vitaniita wataniita mbarikiwa; kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu-na jina lake ni takatifu"(Luka 1:46-49).

EnglishRudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je! Biblia inasema nini kuhusu bikira Maria?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries