settings icon
share icon
Swali

Je! Kuungama dhambi kwa ushirika ni kibiblia?

Jibu


Ungamo la ushirika ni kile kinachotokea wakati jumuiya maalum inapokusanyika kukiri mbele za Mungu dhambi ya pamoja. Mfano unaojulikana sana wa ungamo la ushrika unapatikana katika tangazo la Abraham Lincoln la siku ya kitaifa ya maombi na kufunga: “Tumemsahau Mungu. Tumeusahau mkono wa neema uliotuhifadhi katika amani, na kuzidisha na kututajirisha na kututia nguvu; na tumewaza bila mafanikio, katika udanganyifu wa mioyo yetu, kwamba baraka hizi zote ni kwa sababu ya hekima ya hali ya juu na wema wetu wenyewe. Kwa kulewa kwa mafanikio yasiyokatika, tumejitosheleza sana na kutohisi kulazimika kukomboa na kuhifadhi neema, tukiwa na kiburi cha kumwomba Mungu aliyetuumba! Inatufaa basi, kujinyenyekeza mbele ya Mamlaka iliyochukizwa, kuungama dhambi zetu za kitaifa, na kuomba kwa ajili ya rehema na msamaha” (ilitiwa saini Machi 30, 1863). Katika muda wote wa tangazo hilo, Rais Lincoln anatumia viwakilishi vya wingi kama vile sisi na zetu na kutaja “dhambi za taifa.” Wamarekani waliojiunga katika “siku hiyo ya maombi ya kitaifa na fedheha” walihusika katika kuungama dhambi kwa ushirika.

Kuungama dhambi kwa ushirika ni hadharani, lakini ni tofauti na aina nyingine za maungamo ya dhambi hadharani. Kwa mfano, kuungama dhambi binafsi kunaweza kuhusisha mtu kuja mbele ya jumuiya na mbele za Mungu kuungama dhambi ya kibinafsi au ya siri. Katika maungamo ya ushirika, mtu binafsi huongoza jumuiya katika kuungama hadharani dhambi za kawaida kwa jumuiya hiyo. Kuungama kwa ushrika hakuamrishwi katika Biblia, lakini kunaonyeshwa kama njia ifaayo ya toba ya jumuiya na unyenyekevu mbele za Mungu.

Mungu anathibitisha kuungama dhambi kwa ushirika kama kielelezo kwa Wayahudi katika 2 Mambo ya Nyakati 7:14, “kama watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wangu na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao na nitaiponya nchi yao.” Mungu alisema maneno haya kwa Sulemani katika muktadha wa kuwekwa wakfu kwa hekalu la Yerusalemu. Mungu hakuwa akiweka muundo wa kiliturujia; bali, Alikuwa anasisitiza kanuni ya rehema juu ya jamii inayoishi kwa unyenyekevu mbele zake.

Mfano wa wazi kabisa wa ungamo la ushirika katika Biblia unapatikana katika Ezra 9-10. Ezra amekwisha gundua dhambi kubwa za Israeli ambazo zilitia unajisi jumuiya kwa ujumla. Hasa, wanaume Waisraeli walikuwa wamechukua wanawake wa kipagani kutoka mataifa yaliyowazunguka kama wake zao, na ndoa kama hizo zilikatazwa waziwazi na Mungu (Kumbukumbu 7:3). Ezra anakuja kwa Mungu akilia na kuungama dhambi ya watu: “dhambi zetu zimejikusanya hata kupita juu ya vichwa vyetu na hatia yetu imefika mbinguni….Kwa maana tumedharau maagizo uliyoyatoa kupitia watumishi wako manabii” (Ezra 9:6,10-11). Akiwa anasali hekaluni, kundi kubwa la watu likaungana naye kulia na kuungama dhambi zao. Ni muhimu kutambua kwamba ungamo la kibiblia daima huambatana na majuto ya kweli na toba. Kutaja dhambi tu sio maungamo kamili. Katika hali hii katika kitabu cha Ezra, watu hufualia kilio chao na kuungama dhambi kwa kupanga na kutekeleza mpango wa kuwafukuza wake wa kigeni, waliokatazwa.

Mfano mwingine mashuhuri wa ungamo la ushirika wapatikana katika kitabu cha Yona: “Watu wa Ninawi wakamwamini Mungu, wakatangaza kufunga, watu wote kuanzia mkubwa sana hadi yule mdogo kabisa, wakavaa nguo za gunia. Habari zilipomfikia mfalme wa Ninawi, aliondoka kwenye kiti chake cha enzi, akavua majoho yake ya kifalme, akajifunika nguo ya gunia kisha akaketi chini mavumbini. Ndipo akatoa tangazo katika Ninawi yote: “Kwa amri ya mfalme na wakuu wake: “Msiruhusu mtu yeyote au mnyama, makundi ya ngʼombe au wanyama wengine wafugwao, kuonja kitu chochote, msiwaruhusu kula wala kunywa. Bali wanadamu na wanyama wafunikwe kwa nguo za gunia. Kila mmoja afanye hima kumwomba Mungu. Waziache njia zao mbaya na udhalimu ulio mikononi mwao. Ni nani ajuaye? Huenda Mungu akaghairi kwa huruma yake akaacha hasira yake kali ili tusiangamie’” (Yona 3:5-9). Tena, katika kisa cha Ninawi, jumuiya mahususi ilifahamishwa juu ya hatia yao mbele za Mungu na kujinyenyekeza hadharani, maungamo ya jumuiya na toba. Ingawa maungamo hayakutajwa hasa katika kifungu, inadokezwa na mwito wa kutubu na “kuacha” uovu na vurugu uliokuwa umeenea sana katika utamaduni wao. Hata katika jumuiya ya wapagani waziwazi, wakati wanapomkiri Mungu, wanakubaliana naye kwamba dhambi yao ni mbaya, na kwa bidii kuacha mifumo yao ya dhambi, Mungu ana huruma.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je! Kuungama dhambi kwa ushirika ni kibiblia?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries