settings icon
share icon
Swali

Ufunuo wa asili ni nini?

Jibu


Ufunuo katika theolojia hurejelea ujumbe unaotoka kwa Mungu ili kifichua ukweli kimhusu Yeye au kuhusu sisi wenyewe na ulimwengu unaotuzunguka. Ufunuo umegawanywa katika vitengo viwili: ufunuo wa asili (au ufunuo wa jumla) na ufunuo maalum.

Ufunuo maalum ni ule unaokuja moja kwa moja kutoka kwa Mungu na umeandikwa katika Maandiko yaloyo na mwongozo wa kiungu. Maudhui ya ufunuo huu ni ukweli ambao hatungeweza kuujua isipokuwa Mungu atuambie moja kwa moja. kwa mfano, Utatu na kuhesabiwa haki kwa neema kwa njia ya Imani katika Kristo isingewezekana sisi peke yetu “kutambua.” Ufahamu wetu wa mambo kama hayo huja tu kupitia ufunuo maalum. Ikiwa mtu au kikundi cha watu hakina uwezo wa kupata Biblia katika lugha yao wenyewe, watakuwa hawajui ukweli ambao unaweza kujulikana tu kuptia ufunuo maalum.

Ufunuo wa asili ni ukweli kumhusu Mungu ambao unaweza kutambuliwa kwa kuutazama ulimwengu unaotuzunguka na kwa kujitazama sisi wenyewe. Ingawa si kila mtu anaweza kupata ufunuo maalum, Biblia inaweka wazi kwamba watu kila mahali wanaweza kufikia ufunuo wa asili na kwamba watu wanawajibika jinsi wanavyoitikia. Ufunuo wa asili unachukulia kwamba mfano wa Mungu na uwezo mantiki wa kiakili bado vyatosha kwa wanadamu walioanguka kupokea na kuelewa ufahamu fulani kumhusu Mungu.

Zaburi 19:1-4 inaashiria utele na ufikiaji wa ufunuo asili:
“Mbingu zatangaza utukufu wa Mungu;
anga ladhihirisha kazi ya mikono yake.
Mchana waupasha habari mchana ufuatao,
usiku waufahamisha usiku ufuatao.
Hamna msemo au maneno yanayotumika;
wala hakuna sauti inayosikika;
hata hivyo, sauti yao yaenea duniani kote,
na maneno yao yafika kingo za ulimwengu.
Mungu ameliwekea jua makao yake angani.”

Mwanzoni mwa kitabu cha Warumi kinaelezea ufunuo asili na athari zake:
“Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi na uovu wote wa binadamu ambao kwa njia zao mbaya wanaupinga ukweli usijulikane. Kwa maana, yote yanayoweza kujulikana juu ya Mungu ni wazi kwao; maana Mungu mwenyewe ameyadhihirisha. Tangu Mungu alipoumba ulimwengu, uwezo wake wa milele na uungu wake, ingawa havionekani kwa macho, vinafahamika wazi. Watu wanaweza kuyajua mambo hayo kutokana na vitu hivyo alivyoumba Mungu. Kwa hiyo hawana njia yoyote ya kujitetea!

“Ingawa wanajua kuna Mungu, lakini hawampi heshima anayostahili, wala hawamshukuru. Badala yake, fikira zao zimekuwa batili na akili zao tupu zimejaa giza. Wanajidai kuwa wenye hekima, kumbe ni wapumbavu. Wanaacha kumwabudu Mungu aishiye milele, na badala yake, wanaabudu sanamu zilizo mfano wa binadamu ambaye hufa, mfano wa wanyama, ndege, au wanyama watambaao.”

Kulingana na kifungu cha hapo juu, ufunuo asili ni wa ulimwengu, na wanadamu hupuuza kwa hatari yake mwenyewe. Baadhi ya mambo kuhusu Mungu yanaweza kujulikana kwa kutazama uumbaji (Warumi 1:10). Hasa, mtu anaweza kufahamu kutoka kwa uumbaji kwamba Muumba ana uwezo mkuu na kwamba Yeye ni Mungu-yaani, naastahili kuabudiwa (mstari wa 20). Watu wanapaswa kumshukuru na kumtukuza Muumbaji wa uumbaji wa ajabu (aya ya 21). Ingawa, kifungu hicho pia kinasema kwamba watu hawaitikii ufunuo asili kwa kuabudu au kumshukuru Mungu, na “wasiwe na udhuru” (aya ya 20). Wangefahamu vyema. Mwitikio wa ulimwengu wa wanadamu wenye dhambi si kuanguka chini katika kumwabudu Muumba bali ni kukandamiza ukweli (aya ya 18) na kisha kuabudu na kutumikia viumbe vilivyoumbwa (mstari wa 25), hata kutengeneza mifano ya sanamu yao wenyewe (aya ya 23).

Warumi 1 inaorodhesha idadi ya dhambi ambazo watu wanaokataa na kukandamiza ufunuo asili watajiusisha nazo, hataka kama wanajua kuwa mambo haya ni maovu (aya ya 31). Hawa ni watu ambao hawana sheria ya Mungu iliyoandikwa, lakini wana sheria “iliyoandikiwa mioyoni mwao” (Warumi 2:15). Dhamira ni sehemu ya ufunuo asili. Kuna mambo fulani ambayo watu wanayajua kuwa sawa na mambo mengine kuwa si sahihi. Dhamira inawezakosa, na inaweza potoshwa, lakini wakati watu wanafanya jambo ambalo wanalijua kuwa si sahihi bila hata kuambiwa ni kosa, wanatenda dhambi kwa kukiuka kile ambacho Mungu amewafunulia.

Hatimaye, ufunuo asili unahusishwa na kanuni ya kuwa na msimamo. Warumi 2:1 inasema, “Kwa hiyo huna udhuru wowote, wewe utoaye hukumu kwa mwingine, kwa maana katika jambo lolote unalowahukumu wengine, unajihukumu wewe mwenyewe kwa sababu wewe unayehukumu unafanya mambo hayo hayo.” Ikiwa mtu anaona mtu mwingine anafanya jambo fulani na akafikiri ni kosa, halafu baadaye akafanya jambo lile lile na kulihalalisha, anaasi namna ya ufunuo wa asili.

Swali linaloulizwa mara kwa mara, “Ni nini kitatokea wale ambao hawajawahi kusikia kuhusu Yesu? Je! watahukumiwa kwa kutoamini kwa yule ambaye hawajawahi kusikia juu yake?” jibu ni “Hawatahukumiwa kwa upumbavu wao, lakini watahukumiwa kwa habari waliyopewa.” Na kila mtu amepokea habari nyingi. Uumbaji huonyesha kwamba Mungu ana nguvu na anastahili kuabudiwa. Watu watahukumiwa iwapo walimwabudu Muumba au la. Dhamira inaonyesha kuwa mambo fulani si sawa. Watu watahukumiwa kama walifanya au hawakufanya yale mambo walifikiria si sahihi. Kanuni ya kuwa na msimamo huonyesha kuwa mara nyingi watu hutumbua matendo maovu kwa wengine na kuhalalisha maovu hayo hayo maishani mwao wenyewe. Watu watahukumiwa kulingana na kiwango walichokitumia kuwahukumu watu wengine.

Wakati yote yamesemwa na kutendwa, Maandiko yako wazi juu ya hukumu hii: “Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja. Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu, hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wote wameoza pamoja; hakuna atendaye mema, naam, hakuna hata mmoja. Makoo yao ni makaburi wazi; kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu. Sumu ya nyoka iko midomoni mwao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu. Miguu yao ina haraka kumwaga damu; maangamizi na taabu viko katika njia zao, wala njia ya amani hawaijui. Hakuna hofu ya Mungu machoni pao” (Warumi 3:10-18). Hakuna aneyefuata sheria ya Mungu vile imefunuliwa kwao, iwe ni kupitia ufunuo maalum au ufunuo asili. Wakati wote wamehukumiwa kulingana na kile kimefunuliwa kwao, wote watapatikana na hatia, na hukumu itakuwa ya haki. “Watu wote waliotenda dhambi pasipo sheria wataangamia pasipo sheria, nao wote wale waliotenda dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria” (Warumi 2:12).

Ufunuo wa asili ni sheria, na sheria huhukumu tu. Hakuna atakayeokolewa kwa kushika sheria kwa sababu hakuna awezaye kushika sheria. Tumaini pekee la wokovu ni imani katika Yesu Kristo. Ingawa hakuna anayeshika sheria ya Mungu kama inavyofunuliwa katika ufunuo wa asili kikamilifu, kuna hadithi nyingi za kimisheni za watu ambao wameangalia maisha yao na kutambua kwamba lazima kuwe na Mungu ambaye amesababisha hayo yote, na wamemlilia. Mungu kwa neema Yake, alituma mjumbe kwao kuwaelezea juu ya Yesu, kwa maana hakuna awezaye kuokolewa isipokuwa kumwamini Yeye.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Ufunuo wa asili ni nini?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries