settings icon
share icon
Swali

Je! Ni makosa kwa Mkristo kuwa na mawazo ya ngono?

Jibu


Njozi ni kitendo au tukio linaloundwa katika mawazo; katika hali nyingi tendo linalofikiriwa haliwezekani au si yamkini. Njozi ya ngono huunda tendo la ngono au tukio katika mawazo. Kulingana na asili ya njozi na wahusika wanaofikiriwa, njozi ya ngono inaweza kuwa dhambi. Hali yoyote inayofikiriwa isiyofaa kwa sababu za kitabia, kimaadili, au sababu za kiroho ni dhambi.

Mawazo ni zawadi kutoka kwa Mungu, na njozi ni sehemu ya akili ya mwanadamu. Tunaweza kuwa na njozi mara kwa mara bila hata kutambua. Njozi zinaweza kuanzia kuwaza kwamba haikutulazimu kusimama foleni dukani na kumaliza shughuli zetu mapema, hadi kutunga vitendo viovu na visivyowezekana. Njozi kwa kawaida hutokana na uhalisia wetu wa kibinafsi na ni majaribio ya kuunda ukweli tunaopendelea badala ya ule uliopo. Baadhi ya watu hujiingiza sana katika maisha yao ya njozi hivi kwamba hujitenga na ukweli na mahusiano halisi. Baadhi ya chaguo za mtandao huruhusu watu kuunda wahusika na kuishi kwa ubinafsi kupitia wahusika hao. Njozi za ngono mara nyingi ni sehemu ya ukweli huo wa mtandaoni na huwaruhusu watu kuiga vitendo vya ngono bila kuwepo kihalisi.

Mithali 23:7 inasema kwamba chochote tunachofikiri mioyoni mwetu, ndivyo tulivyo. Wengi wanaweza kubishana, “Lakini sifanyi chochote kibaya.” Hata hivyo, Biblia inazungumza mengi kuhusu mawazo yetu na ni wazi kwamba tunapaswa kuyasalimisha mawazo yetu chini ya mapenzi ya Mungu. Yesu alisema, “Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi. Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio” (Mathayo 15:18-19). Pia alisema kwamba, hata ukimtazama mtu kwa tamaa ni kama dhambi ya uzinzi (Mathayo 5:28). Ikiwa njozi ya ngono inajumuisha matendo au maneno ambayo hayaambatani na mapenzi ya Mungu kwetu, basi ni dhambi. Mawazo ya kingono kuhusu wenzi wetu wa ndoa yanaweza yasiwe dhambi, ikiwa tuko huru kiadili kutenda kulingana na mawazo hayo. Lakini ikiwa tunawaza juu ya kushiriki tendo la ndoa na mtu ambaye hatujafunga naye ndoa, hio ni tamaa. Na tamaa ni dhambi.

Hatuwezi kudhibiti mawazo yetu kila wakati. Tunakumbana na vichochezi vya ngono kila mara, na wanaume hasa wana wakati mgumu kukabiliana na vichocheo hivi kwa njia za kumtukuza Mungu. Andiko la Waefeso 6:16 linazungumza kuhusu “mishale yote yenye moto ya yule mwovu.” Shetani hulenga akili zetu kwa mishale hiyo, na fikira za ngono ni mojawapo ya mishale yenye moto ambayo, ikiachwa bila kupingwa inaweza kutuingiza katika dhambi. Yakobo 1:13-15 inatuonyesha jinsi dhambi inavyokua, kuanzia na “tamaa mbaya.”

Wakati tamaa zinapochipuka mioyoni mwetu, tuko na chaguo la kufanya kuzihusu. Tunaweza kuziitikia, kuzikubalia kuchipuka na kuwa njozi, au tunaweza “kuteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo” (2 Wakorintho 10:5). Kama Wakristo, tuko na nguvu za Roho Mtakatifu zinazofanya kazi katika maisha yetu ili kutuwezesha kukomesha njozi isiyo ya Kiungu linapoanza. Tunapotambua kuwa tunaota ndoto za mchana kuhusu jambo ambalo Mungu amesema hatupaswi kulifikiria, tunaweza kulikamata haraka wazo hilo, kulikiri kwa Yesu, na kuomba msamaha Wake (1 Yohana 1:9). Kadri tunavyoendelea kutumia aina hii ya kusimamsiasha mawazo, basi hatutahisi kutojiweza wakati mawazo yetu yanapojaribu kutupoteza.

Baadaye, inaweza kuwa jambo la kusaidia kuchunguza aina ya njozi ambayo inaonekana kutawala mawazo yako. Njozi mara nyingi hufunua mahitaji ambayo hayajatimizwa ambayo Mungu anataka kukimu kwa njia bora. Vivyo hivyo, mawazo ya ngono yanaweza kuonyesha mahali palipojeruhiwa katika roho zetu ambapo Mungu anahitaji kuponya. Mawazo hayo yakiendelea na kusumbua, kutafuta shauri la kimungu kunaweza kusaidia kufichua mizizi ya jeraha la moyo inayoyasababisha. Tunapokuwa na shaka kuhusu fikira za ngono au wazo lingine lolote lenye kuchosha, tunaweza kurejelea Wafilipi 4:8 ili kuona kama linampendeza Mungu. Anataka kuwa Bwana wa kila sehemu yetu, hii ikiwa ni pamoja na njozi zetu.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je! Ni makosa kwa Mkristo kuwa na mawazo ya ngono?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries