settings icon
share icon
Swali

Mungu mwenye upendo anawezaje kumtuma mtu kuzimu?

Jibu


Ili kushughulikia swali la Mungu mwenye upendo kumtuma mtu kuzimu, tunahitaji kufafanua maneno machache na kusahihisha dhana chache sisizo sahihi. Ufafanuzi wetu lazima uwe wa kibiblia, na dhana zetu lazima ziwe sahihi.

Kwanza ni lazima tufafanue maneno Mungu mwenye upendo. Kifungu hiki cha maneno kinachukulia kawaida baadhi ya mambo kuhusu Mungu, na kujibu swali lililopo kulingana na mawazo yenye dosari husababisha hitimisho lisilo sahihi. Utamaduni wetu unafafanua “Mungu mwenye upendo” kama kiumbe asiye na migogoro kabisa ambaye anavumilia chochote tunachotaka kufanya. Lakini huo si ufafanuzi wa Kibiblia. Yohana wa kwanza 4:16 inasema kwamba Mungu ni upendo. Hiyo ina maana kwamba Yeye hamiliki upendo kama sisi; Yeye ndiye ufafanuzi hasa wa upendo na kwa hivyo hawezi kufanya chochote kisicho na upendo. Sheria ya kutopingana inasema kwamba jambo haliwezi kuwa kweli na sio kweli kwa wakati mmoja. Kwa hivyo, ikiwa Mungu ni upendo, basi hawezi kuwa vile vile Mungu asiye na upendo.

Kwa hivyo uongo uliopo katika swali “Mungu mwenye upendo anawezaje kumpeleka mtu kuzimu?” ni wazo la kwamba kuruhusu watu waende motoni ni tendo lisilo na upendo kwa upande wa Mungu. Ikiwa sisi wanadamu tutaamua kwamba Mungu amekosea kwa njia fulani kuruhusu watenda-dhambi wasiotubu walipe adhabu inayostahili, basi tumetangaza kwamba sisi ni wenye upendo ziadi kuliko Mungu. Tumejifanya kama mahakimu wa Mungu na kwa kufanya hivyo tumefunga mlango wa ufahamu wa kina. Kwa hiyo, hatua ya kwanza katika kujibu swali hili ni kukubaliana na Maandiko kwamba Mungu Ni upendo; kwa hivyo, kila kitu Anachofanya ni onyesho la upendo huo mkamilifu.

Uwongo wa pili unatolewa na swali “Mungu mwenye upendo anawezaje kumtuma mtu motoni?” unahusu neno kutuma, ambalo huashiria kitendo tu kwa upande wa mtumaji. Mtu akituma barua, kutuma ombi, au kutuma zawadi, hatua zote zilifanywa na mtu huyo. Hakuna hatua iliyochukuliwa kwa upande wa barua, ombi, au zawadi. Hata hivyo, ufahamu huu wa neno kutuma hauwezi kutumika kwa swali lililopo kwa sababu Mungu amewapa wanadamu uhuru wa kushiriki katika uchaguzi wao wa maisha na hatima za milele (Yohana 3:16-18). Jinsi swali hili limeundwa inadokeza kwamba, ikiwa mtu yeyote ataenda kuzimu, ni matokeo ya kitendo cha Mungu cha upande mmoja, na mtu anayepelekwa kuzimu ni mhasiriwa tu. Wazo kama hilo linapuuza kabisa wajibu wa kibinafsi ambao Mungu amekabidhi kwa kila mmoja wetu.

“Ni namna gani Mungu mwenye upendo anawezaje kumtuma mtu kuzimu?” swali lote zima si sahihi. Maneno bora zaidi ni “Ikiwa Mungu ni upendo, basi kwa nini watu fulani huenda motoni?” Warumi 1:18-20 huweka msingi wa jibu hili: “Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

Kunayo mambo kadhaa muhimu katika kifungu hiki ambayo kwa kiasi fulani yanatuonyesha moyo wa Mungu. Kwanza ni ukweli kwamba watu “wanakandamiza ukweli” kwa bidii. Watu wamepewa ukweli wa kutosha kujua na kujisalimisha kwa Mungu, lakini wanaukataa. Nia ya kibinafsi inataka kukataa haki ya Mungu ya kutuambia la kufanya. Kwa hiyo, wakiwa na ukweli mbele yao, watu wengi hukengeuka na kukataa kuuona. Thomas Nagel asiyeamini kuwa kuna Mungu amesema, “Sio kwamba tu siamini katika Mungu, na kwa kawaida ninatumaini kwamba niko sahihi katika imani yangu. Ni kwamba ninatumaini hakuna Mungu! Sitaki kuwe na Mungu; sitaki ulimwengu uwe hivyo.”

Pili, Warumi sura ya 1 inasema kwamba Mungu ‘anayafanya yajulikane kwao.” Kwa maneno mengine, Mungu amechukua hatua ya kufanya ukweli Wake ujulikane kwa kila mtu. Historia imethibitisha hilo tangu wakati ulipoanza, kwa kuwa kila kikundi cha watu kimetafuta ufahamu fulani juu ya Muumba ambaye wanapaswa kumtii. Ufahamu kama huo ni sehemu muhimu ya maana ya kuumbwa kwa mfano wa Mungu (Mwanzo 1:27). Kisha Warumi 1:20 husema kwamba “watu hawana udhuru.” Na wangempa nani kisingizio kama hicho? Yeye ambaye anasema amejitambulisha kwao, laiti wengenyenyekea na kukubali ufunuo kama huo. Mungu anahukumu kila mmoja wetu kulingana na ukweli ambao ametupatia, na Warumi 1 inasema kwamba kila mmmoja wetu ana ukweli wa kutosha wa kumrudia badala ya kusonga mbali Naye.

Tunapojibu swali “Mungu mwenye upendo anawezaje kumtuma mtu motoni?” sehemu nyingine ya asili ya Mungu inatumika. Mungu si upendo tu, bali ni mkamilifu na mwenye haki pia. Haki inahitaji malipo ya kutosha kwa uhalifu uliofanywa. Adhabu pekee ya haki kwa uhaini mkubwa dhidi ya Muumba wetu mkamilifu ni kutengwa naye milele. Utengano huo unamaanisha kutokuwepo kwa wema, nuru, uhusiano, na furaha, ambazo zote ni sehemu za asili ya Mungu. Kutoa udhuru kwa dhambi yetu kungehitaji Mungu kuwa asiye wa haki na kuruhusu wanadamu waliochafuliwa na dhambi kuingia mbinguni Yake kamilifu kungefanya mahali hapo kusiwe kamilifu. Ndiyo sababu Mwana mkamilifu wa Mungu pekee ndiye angeweza kwenda msalabani badala yetu. Damu yake kamilifu pekee ndiyo ilikuwa malipo yanayokubalika kwa deni ambalo kila mmoja wetu anadaiwa na Mungu (Wakolosai 2:14). Tunapomkataa Yesu kama mbadala wetu, lazima tulipe gharama sisi wenyewe (Warumi 6:23).

Mungu alitupa uhuru wa kuchagua jinsi tunavyomwitikia. Ikiwa angetulazimisha kumpenda, tungekuwa roboti. Kutotupa chaguo ila utiifu itakuwa ni ukiukaji wa hiari yetu. Upendo ni upendo tu wakati ni wa hiari. Hatuwezi kumpenda Mungu tusipokuwa na chaguo la kutompenda. Kwa sababu Mungu anaheshimu uhuru wetu, hatalazimisha kujisalimisha au uaminifu. Walakini, kuna matokeo kwa chaguo lolote. C. S. Lewis anatoa muhtasari wa ukweli huu katika kitabu chake maarufu, Talaka Kuu (The Great Divroce): “Kuna aina mbili tu ya watu mwishowe: wale wanaomwambia Mungu, “Mapenzi yako yatimizwe,’ na wale ambao Mungu atawaambia, mwishowe, ‘Mapenzi yako yatimizwe,’ Wale wote walio kuzimu, wanachagua hili.”

EnglishRudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Mungu mwenye upendo anawezaje kumtuma mtu kuzimu?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries