settings icon
share icon
Swali

Mnyama katika Ufunuo ni nani?

Jibu


Wakati wa kipindi cha dhiki, ulimwengu utatawaliwa na mtu asiyemcha Mungu, akiongoza mfumo ovu wa serikali. Biblia inahusisha mtawala huyu wa nyakati za mwisho na mnyama wa kutisha katika kitabu cha Ufunuo na kitabu cha Danieli.

Katika Ufunuo 13 Yohana anaona maono ya kutisha ya joka mmoja na wanyama wawili. Mnyama wa kwanza anatokea baharini na anapokea mamlaka kutoka kwa joka au Shetani. Mnyama huyo ni wa kutisha: “mwenye pembe kumi na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru. Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dabu, na kinywa chake kama kinywa cha simba” (Ufunuo 13:1-2). Maono ya Danieli ya mnyama yanafanana kwa njia mingi na maono ya Yohana (Danieli 7:7-8,19-27). Kuvidadisi vitabu vya Danieli na Ufunuo kwa mkabala ni kwa manufaa sana.

Katika Ufunuo, neno mnyama linarejelea viumbe viwili vinavyohusiana. Wakati mwingine neno “mnyama” limetumika likirejelea milki za nyakati za mwisho. Vichwa saba na pembe vinaonyesha kuwa mnyama atakua ni muungano wa mataifa ambayo yanayoinuka kwa mamlaka na kutishia dunia iliyo chini ya utawala wa Shetani. Marejeleo ya neno “mnyama” katika Ufunuo yanaashiria mtu-mtu ambaye ni kiongozi wa kisiasa na anayetawala milki ya uhayawani.

Mnyama huyo atapata jeraha la mauti na ataponywa (Ufunuo 13:3). Atakuwa na mamlaka juu ya ulimwengu wote na kutaka kuabudiwa (Ufunuo 13:7-8;) Atapigana vita na watu wa Mungu na kuwashinda kwa muda (Ufunuo 13:7; Danieli 7:21). Hata hivyo, muda wa mnyama huyo utakuwa mfupi sana: kulingana na Ufunuo 13:5 na Danieli 7:25, ataruhusiwa kuwa na mamlaka kikamilifu kwa muda wa miezi arobaini na miwili ( miaka mitatu na nusu).

Tunaamini kuwa mnyama katika kitabu cha Ufunuo ni Mpinga Kristo, yule ambaye ni “mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi kana kwamba yeye ndiye Mungu” (2 Wathesalonike 2:4). Pia anaitwa “mtu wa uasi” na “mtu ambaye amehukumiwa kuangamizwa” (2 Wathesalonike 2:3). Katika maono ya Danieli, Mpinga Kristo ni “pembe ndogo” ambayo inachibuka kichwani cha ule mnyama wa kutisha (Danieli 7:8).

Bwana atakaporejea kwa hukumu, atamshinda yule mnyama na kuangamiza ufalme wake (Ufunuo 19:19-20; tazama pia Danieli 7:11). Yule mnyama atatupwa katika ziwa la moto akiwa hai. Bado utambulisho wa mtu atakaye kuwa mnyama wa Ufunuo haujulikani. Kulingana na 2 Wathesalonike 2:7 mtu huyu atafunuliwa tu wakati Mungu atakapoondoa ule ushawishi unaozuia Roho Mtakatifu kutoka duniani.

Ni jambo la kufurahisha kulinganisha maono ya kibiblia yanayotofautiana kuhusu falme za kidunia. Katika Danieli 2, Mfalme Nebukadneza aliota kuhusu falme za ulimwengu kuwa kama “sanamu kubwa, kubwa mno kupita kiasi, sanamu iliyongʼaa na yenye sura ya kushangaza” (Danieli 2:31). Nabii Danieli baadaye aliona maono sawia ya falme kama hizo, isipokuwa anaziona kuwa mnyama mwenye sura ya kutisha (Danieli 7). Katika maono ya Yohana kuhusu falme za mwisho za kidunia, milki inadhihirishwa kuwa mnyama mwenye sura mbaya na aliyeumbika vibaya. Vifungu hivi vinaonyesha mitazamo miwili ya falme ambazo mwanadamu uhunda. Mwanadamu huona kuwa ubunifu wake ni wa kuvutia na kazi yake ya usanaa kuwa ya madini ya dhamani. Walakini maoni ya Mungu kwa falme hizo hizo ni kwamba ni sanamu zisizo za kiasili. Na mnyama wa Ufunuo atakuwa mbaya zaidi kuliko wengine wote.

English

Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Mnyama katika Ufunuo ni nani?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries