settings icon
share icon
Swali

Je, inamaanisha nini kuwa na mfano wa utauwa lakini kukana nguvu zake?

Jibu


Katika 2 Timotheo 3, mtume Paulo anaeleza hali ya watu katika siku za mwisho. Katika maelezo yake, anaonya juu ya watu ambao wana sifa ya kuwa na “ mfano wa utauwa kwa nje, lakini wakizikana nguvu za Mungu” (msitari wa 5). Kisha Paulo anatoa amri hii: “Jiepushe na watu wa namna hiyo.”

Mara nyingi Paulo hutumia utofautishaji ili kusisitiza sifa anayotaka kuangazia. Katika 2 Timotheo 3:1-4, anampa Timotheo orodha ndefu ya tabia za dhambi na mitazamo ambayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu. Katika mstari wa 5 anamwambia Timotheo ajiepushe na wale wanaosema kwamba wao ni Wakristo kwa vinywa vyao-wana “mfano” wa utauwa-lakini wanaotenda kama wasioamini- wanakana nguvu ya utauwa.

Wale walio na mfano wa utauwa ni wale wanaofanya maonyesho ya nje ya dini. Wanajionyesha kuwa wacha Mungu, lakini yote ni kwa ajili ya kujionyesha. Hakuna nguvu katika dini yao kama vile inavyothibitishwa na ukweli kwamba maisha yao hayabadiliki. Wanazungumza juu ya Mungu na kuishi katika dhambi, na wako sawa na mpango huo.

Wakristo hawa wa uwongo ni waharibifu. Paulo anaonya kwamba, “Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya” na kwamba “Wanajifunza siku zote lakini kamwe wasiweze kufikia ujuzi wa kweli” (2 Timotheo 3:6-7). Anawalinganisha na waganga waovu waliompinga Musa na kuonya kwamba upumbavu wao na akili zao potovu zitafichuliwa kwa wote hatimaye (mistari ya 8-9).

Nguvu ya Mungu ambayo inapaswa kuandamana na namna ya utauwa, inaonyeshwa kwa njia ya Roho Mtakatifu na matokeo katika mabadiliko ya maisha yetu. Roho Mtakatifu hukaa ndani ya muumini (1 Wakorintho 6:19) na kumwezesha kuzaa matunda bainifu: upendo, furaha, Amani, uvumilivu, utu wema, Fadhili, uaminifu, upole, na kiasi (Wagalatia 5:22-23). Hizi ndizo sifa za Mkristo wa kweli, kinyume na orodha ya Paulo ya dhambi katika 2 Timotheo 3:1-4.

Ushauri wa Pualo kwa Timotheo unaafikiana na maelezo ya Yakobo jinsii ya kutambua imani ya kweli (Yakobo 2:14-26). Imani ya kweli itathibitishwa na matendo mema, ambayo yatatokea kwa kawaida. Ikiwa mtu anasema yeye ni Mkristo lakini haonyeshi ushahidi katika maisha yake kwa kuzaa tunda la Roho, inatubidi kufanya hukumu juu yake na kuepuka mtu huyo. Anaweza kuwa na namna ya utauwa, lakini anakana nguvu za Mungu kwa kutojiruhusu kutawaliwa na Roho. Kwa kweli, ikiwa imani yake si ya kweli, hawezi kutawaliwa na nguvu za Mungu, kwa sababu Roho Mtakatifu hakai ndani yake.

“Mtu ambaye hana Roho hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa upambanuzi wa rohoni” (1 Wakorintho 2:14). Mtu wa kawaida anaweza kuwa na namna ya utauwa, lakini anakana nguvu za Mungu kulingana na vile anavyoishi. Imani katika Yesu Kristo pekee ndiyo inayoweza kuleta kuhesabiwa haki na mabadiliko anayohitaji sana (Wakolosai 1:21-22; Warumi 5:1-2).

EnglishRudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je, inamaanisha nini kuwa na mfano wa utauwa lakini kukana nguvu zake?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries