settings icon
share icon
Swali

Je, ninawezaje kuyaondoa mawazo ya tamaa?

Jibu


Tanmaa ni hitaji lolote lenye nguvu; tamaa ya dhambi ni tamanio la kitu ambacho Mungu amekataa. Mawazo ya tamaa huzaa matendo ya tamaa, na tamaa inayotendwa daima husababisha uharibifu. Hawa alitamani tunda la kupendeza kutoka kwa mti mmmoja ambao Mungu alikuwa amesema, “Wasile matunda yake” (Mwanzo 2:16-17). Kitendo chake cha kula na kumpa mumewe tunda kilifungua mlango wa dhambi kuingia katika ulimwengu mkamilifu wa Mungu. Daudi alimtamani Bathsheba, mke wa mtu mwingine, na alipotenda kulingana na tamaa hiyo, ilisababisha mauaji na kifo cha mtoto wake mchanga, kama sehemu ya hukumu ya Mungu (2 Samweli 11:2-4, 14-15; 12:13014). Matendo maovu huanza na mawazo ya tamaa, kwa hivyo ni muhimu tuondoe mawazo haya mara tu yanapofika.

Ili kuyaondoa mawazo ya tamaa, lazima kwanza tufafanue maeneo yetu makubwa zaidi ya majaribu. Sio kila wakati tamaa huwa ya ngono. Uchoyo ni tamaa ya pesa au madaraka. Wivu ni tamaa ya umaarufu au nafasi ambayo mtu mwingine anayo. Shauku ni tamaa ya kitu chochote ambacho hatuna. Tamaa huanza na wazo. Ingawa hatuwajibiki kwakila wazo linaloingia vichwani mwetu, tunawajibika kwa kile tunachofanya na mawazo hayo.

Samweli wa Pili 13 inasimulia kisa cha kuhuzunisha cha mawazo ya ashiki yanayogeuka kuwa matendo maovu. Amnoni, mwana wa Mfalme Daudi, alimtamani sana Tamari dadaye wa kambo. Kwa sababu hakuyashinda mawazo yake ashiki, yalimlemea hadi akafanya kitendo cha kutisha cha kumbaka. Baada ya tamaa yake kutosheka, hakujali tena kilichompata Tamari, alimtema nje kama takataka (aya ya 15). Tamaa hujali tu kikidhi matakwa yake, haijali chochote kuhusu watu wanoumizwa nayo. Wazo la tamaa lapaswa kuonekana kama adui kabla litawale maisha yetu.

Wakati tunashikilia wazo ambalo tunajua kwamba halimpendezi Mungu, linaweza kuwa tamaa ya dhambi haraka. Hamu hukua na kusababisha kutoridhika na hali yetu ya sasa. Tamaa hutufanya kuamini kwamba furaha na kutosheka haviwezekani isipokuwa tuwe na kile tunachotaka. Yakobo 1:13-15 inaelezea ukuaji wa wazo la tamaa na kuwa tendo la tamaa: “Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu yeyote.Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya. Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba, huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa, huzaa mauti.”

Tunaweza kuondokana na mawazo ya tamaa kwa kuyabadilisha na mawazo yaliyo “ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo” (Wafilipi 4:8). Ni lazima “tuteke nyara kila fikira ipate kumtii Kristo” (2 Wakorintho 10:5). Ni lazima tutubu kwa kukubali mawazo ya tamaa na kumuuliza usaidizi wa Bwana katika kuyaelekeza mawazo yetu.

Ikiwa mawazo ya tamaa tunayojabiru kuyaondoa yanahusisha mtu mwingine, tunaweza kupunguza nguvu zake kwa kugeuza mawazo hayo kuwa maombi kwa ajili ya ustawi wa mtu huyo. Kwa kumleta mtu huyo mbele za Bwana, tunadhoofisha nguvu ya tamaa ya kumdhalilisha. Ni lazima tutambue thamani ya kila mtu kama kiumbe wa Mungu na kukumbuka kwamba Mungu ana mipango ya juu zaidi kwa ajili yake ambayo haitujumuishi. Mapenzi yetu yanapokubaliana na mapenzi ya Mungu, tunajifunza kumwona mtu huyo vile Yeye anavyomwona, si kama vile tamaa inavyofanya.

Kukomesha mawazo ya tamaa huitaji kuichunguza habari tunayoiruhusu kuingia akilini mwetu kupitia hisia zetu. Mawazo yetu kwa kawaida huwa ni matokeo ya yale ambayo tumeona, kusikia, kuguza na kuonja. Kwa kudhibiti kile tunachoruhusu, tunaweza kupunguza sana mambo yanayopatikana katika akili zetu ili tamaa isiyatumie vibaya. Ikiwa picha za ponografia zimeingizwa katika akili zetu kupitia kuzitazama tunaweza kumwomba Bwana abadilishe picha hizo muda baada ya muda. Kwa kukataa kutazama vitu vinavyoamsha tamaa, kuchagua muziki na lugha ambayo hujenga mawazo ya tamaa, na kupiga marufuku kumbukumbu za tamaa kutoka kwa mkusanyiko wetu, tunaweza kupunguza mawazo ya tamaa hadi yasipate nafasi ya kufanya kazi.

Kukariri na kutafakari Maandiko pia ni njia nzuri ya kuepuka mawazo ya tamaa na kufanya upya akili zetu kama Warumi 12:1-2 inavyotuagiza kufanya. Kucheza muziki wa kuabudu masikioni mwetu pia huelekeza akili zetu kwenye yale yaliyo mema, safi na mazuri. Maisha ya Mkristo ni yakujisalimisha kila mara. Tunapojisalimisha kila siku kwa ukuu wa Kristo, Yeye hutusaidia kubadilisha maisha ya mawazo ya dhambi kuwa yale yanayomfuata Yeye. Mawazo yenye tamaa hutuvamia sote mara kwa mara, lakini kuchukua mamlaka juu yao, kuyakataa kabla ya kuota mizizi, na kutafuta msaada wa Mungu kunaweza kutupa ushindi.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je, ninawezaje kuyaondoa mawazo ya tamaa?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries