settings icon
share icon
Swali

Tunaweza kujifunza nini kutokana na maombi ambayo Yesu aliomba?

Jibu


Maombi ambayo Yesu aliomba yanatupa ufahamu wa asili Yake, moyo Wake, na utume Wake duniani. Maombi ya Yesu pia yanatufahamisha na kututia moyo katika maisha yetu ya maombi. Muhimu zaidi kuliko mahali Aliomba, wakati Alipoomba, na Aliomba akiwa katika mkao gani, ukweli ni kwamba Aliomba. Maudhui ya maombi yake ni mafundisho kwa ajili yetu sote.

Maombi yalikuwa sehemu muhimu ya wakati wa Yesu duniani, na Aliomba mara kwa mara: “Lakini mara kwa mara Yesu alijitenga nao ili kwenda mahali pa faragha kuomba” (Luka 5:16). Ikiwa Mwana aliyefanyika mwili aliona ni muhimu kuzungumza na Baba mara kwa mara, je, ni kiasi gani zaidi tunahitaji kufanya hivyo? Yesu alikabili mateso, majaribu, maumivu ya moyo, na kuteseka kimwili. Bila kufikia mara kwa mara wa kiti cha enzi cha Mungu, hakika angepata mambo hayo kuwa yasiyoweza kustahimili. Vivyo hivyo, Wakristo hawapaswi kamwe kupuuza “tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji” (Waebrania 4:16).

Kile ambacho mara nyingi huitwa “Sala ya Bwana” kwa hakika ni chombo cha Kristo cha kufundishia kama sehemu ya Mahuribi Yake ya Mlimani (Mathayo 6:9-13). Katika sala hiyo ya kielelezo, Yesu anatufundisha kumkaribia Mungu kama “Baba yetu”; kuliheshimu jina la Mungu; kuomba mapenzi ya Mungu yafanyike; na kuomba riziki yetu ya kila siku, msamaha, na ulinzi wa kiroho.

Zaidi ya nyakati Zake za kawaida za maombi, Yesu aliomba katika matukio muhimu maishani Mwake: Aliomba wakati wa ubatizo Wake (Luka 3:21-22); kabla ya kuwalisha 5,000 (Luka 9:16) na 4,000 (Mathayo 15:36); na wakati wa kubadilika kwake kwa asura (Luka 9:29). Kabla ya Yesu kuwachagua wanafunzi wake kumi na wawili, “alikesha usiku kucha akimwomba Mungu” mlimani (Luka 6:12). Yesu aliomba wakati wanafunzi 72 waliporudi: “Wakati huo Yesu akashangilia katika Roho Mtakatifu, akasema, ‘Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza” (Luka 10:21).

Yesu aliomba kwenye kaburi la Lazaro. Walipoondoa jiwe kwenye kaburi la rafikiye, “Yesu akainua macho yake juu akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia. Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya umati huu uliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma’” (Yohana 11:41-42). Huu ni mfano mzuri wa maombi yaliyoombwa katika masikio ya wengine kwa ajili ya wasikilizaji.

Huko Yerusalemu juma la kukamatwa kwake, Yesu alitabiri kifo chake ambacho kilikaribia. Alipozungumza kuhusu dhabihu yake inayokuja, Yesu alisali sala fupi sana: “Baba, litukuze jina lako” (Yohana 12:28). Kwa mwitikio kwa sala ya Yesu, sauti kutoka mbinguni ilisema, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.” Akitumia muda wake mfupi na wanafunzi Wake katika usiku wa kukamatwa kwake, Yesu aliomba sala ndefu inayojulikana hii leo kama “sala Yake ya ukuhani mkuu” (Yohana 17) kwa niaba ya wana wake mwenyewe, wale aliopewa na Baba (mstari wa 6). Katika maombi haya, Yesu ndiye mwombezi wa watoto wake (rejelea Waebrania 7:25). Anasali …siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako” (aya ya 9). Anaomba kwamba wawe na furaha Yake (mstari wa 13) na kwamba Mungu awalinde na yule mwovu (mstari wa 15). Anawaombea walio Wake watakaswe na ile kweli, ambayo ni Neno la Mungu (mstari wa 17), na kuunganishwa katika ukweli huo (mistari ya 21-23). Katika sala ya Yohana 17, Yesu anatazamia wakati ujao na anajumuisha wale wote ambao wangeweza kumwamini (mstari wa 20).

Yesu aliomba katika bustani ya Gethsemane kabla kukamatwa kwake (Mathayo 26:36-46). Aliwataka wanafunzi Wake kusali pamoja Naye, lakini badala yake walilala. Sala ya Yesu yenye uchungu katika bustani ni kielelezo cha utii na dhabihu: “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe” (aya ya 39). Yesu aliomba namna hii mara tatu.

Yesu aliomba kutoka msalabani, katikati ya uchungu Wake. Sala yake inaangwi Zaburi 22:1 na inaonesha huzuni yake kuu: ”Ilipofika saa tisa, Yesu akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”) (Mathayo 27:46). Yesu pia aliomba msamaha kwa wale waliokuwa wakimtesa hadi kufa: “Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura” (Luka 23:34). Katika pumzi yake ya mwisho, Yesu anaendelea kuonesha imani yake kwa Mungu: “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu” (Luka 23:46).

Mada nyingi zinaonekana wazi katika sala za Yesu. Moja yao ni kutoa shukrani kwa Baba. Sifa ilikuwa sehemu ya kawaida ya sala za Yesu. Mada nyingine ni ushirika wake na Baba; Uhusiano wake na Baba yake wa mbinguni kwa kawaida ulisababisha hamu Yake ya kutumia wakati kuwasiliana Naye. Dhamira ya tatu katika mombi ya Yesu ni kujisalimisha kwake kwa Baba. Maombi ya Bwana wetu daima yalikuwa sawa na mapenzi ya Mungu.

Kama vile Yesu alivyotoa shukrani, tunapaswa kuomba kwa shukrani katika mambo yote (Wafilipi 4:6-7). Kama watoto wa Mungu walioasiliwa, tunapaswa kutamani kuzungumza na Mungu (Waefeso 3:12). Na katika kila jambo tunapaswa kutafuta mapenzi ya Bwana kuliko yetu wenyewe. Yesu aliomba katika mazingira mbalimbali, hadharani na faraghani. Aliomba wakati wa furaha na nyakati za huzuni. Alijiombea Mwenyewe, na Aliwaombea wengine. Alisali ili kutoa shukrani, maombi ya mahitaji, na kuzungumza na Baba Yake. Yesu aliweka mfano wa jinsi tunavyopaswa kumwamini Mungu, kujinyenyekeza kwa Mungu, na kutafuta ushirika na Mungu.

Hadi hii leo, Yesu anaendelea kusali kwa ajili ya walio Wake kutoka katika cheo Chake kilichoinuliwa mbinguni kwenye mkono wa kuume wa Mungu. Maandiko yanasema Yeye huwaombea walio wake (Waebrania 7:25; Warumi 8:34; 1 Yohana 2:1). Ni muhimu kwamba katika kupaa kwa Yesu, alichukuliwa kutoka kwa wanafunzi Wake kwenda mbinguni “alipokuwa akiwabariki” (Luka 24:51). Baraka hiyo haijawahi kukoma. Yesu ataendelea kuwabariki wale wanaokuja kwa Mungu kupitia imani katika Kristro hadi atakapokuja tena.

EnglishRudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Tunaweza kujifunza nini kutokana na maombi ambayo Yesu aliomba?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries