settings icon
share icon
Swali

Je! Kazi za Shetani katika 1 Yohana 3:8 ni zipi?

Jibu


Waraka wa kwanza wa Yohana 3:8 unatupa sababu kuu ya kuja kwa Yesu ulimwenguni: “Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi.” Shetani alikuwa akijishughulisha sana na kazi yake katika ulimwengu huu, na Mwana wa Mungu alipotokea Shetani akaboresha utendaji kazi wake (ona Mathayo 4:1-11; Luka 4:41). Habari njema ni kwamba nguvu na uwepo wa Yesu huharibu kazi ya Shetani.

Ili kuliweka tamko “kazi za Ibilisi” katika muktadha, ni lazima tusome kile kinachoongoza kwa tamko hilo: “Watoto wapendwa, mtu yeyote asiwadanganye. Kila mtu atendaye haki ana haki, kama yeye alivyo na haki. Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi” (1 Yohana 3:7-8). Mtume Yohana anazungumza juu ya utakatifu wa kibinafsi. Mtoto wa Mungu anaishi katika haki. Wale wanaoishi katika kutotubu, dhambi iliyoendelea hujionyesha kuwa watoto wa ibilisi kwa sababu wanaakisi asili ya Shetani. Yule ambaye Kristo anakaa ndani yake haendelei kutenda dhambi kwa sababu Kristo alikuja kuharibu kazi za Shetani. Kazi hizo za kiShetani hazina usemi tena ndani ya moyo wa muumini. Kristo alikuja kuharibu kazi za Shetani na hiyo inatuhakikishia utakaso wetu.

Kazi za Shetani ni zipi hasa? Vifungu kadhaa katika Biblia vinajibu swali hili, lakini Yesu anatoa jibu la wazi na fupi katika Yohana 8:44. Akiwakabili viongozi wa kidini wanafiki katika Israeli, Yesu asema, “Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo.” Kulingana na Yesu, baadhi ya kazi za Shetani ni kuua na kusema uongo. Dhambi hizi mbili zinatoa muhtasari wa tabia ya Shetani na malengo yake. Anafanya kazi ya kuona kuwa watu wanaangamizwa na kwenda kuzimu (hayo ni mauaji), na anatamani kuwahadaa katika uharibifu huo (ambao ni uongo).

Kazi za ibilisi zinaonekana katika bustani ya Edeni, ambapo Shetani alimdanganya Hawa na kumpeleka katika uasi (mwanzo 3:1-6). Matokeo yake ni, Adamu pia alitenda dhambi na kuwatupa wanadamu wote katika utumwa wa dhambi (Warumi 5:12). Shetani alimdanganya Hawa kwa lengo la kumuua (yaani, kumtenga na Mungu); alitaka ubinadamu ufe.

Kabla hatujaokolewa, tulikuwa chini ya athari kamili za kazi za Shetani. Kwa kweli, “Kwa habari zenu, mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu, ambazo mlizitenda mlipofuatisha namna ya ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii” (Waefeso 2:1-2). Kazi za Shetani maishani mwetu zilitufanya “tutimize tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote” (mstari wa 3). Ni kupitia upendo, rehema, na neema ya Mungu pekee ambapo tuliokolewa kutoka kwa kazi za ibilisi (mistari ya 4-5).

Kazi za Shetani huathiri ubinadamu kimaadili, kimwili, kiakili, na kiroho. Kimaadili, Shetani huwashawishi watu kutenda dhambi, na kufanya uovu uonekane kuwa wa kuvutia ili watu wachague uovu badala ya kumtii Mungu (Yakobo 1:14). Kimwili, Shetani anaweza kusababisha magonjwa, na anatafuta kutumia majariub ya kimwili kuwafanya watu wamlaani Mungu (Ayubu 2:4-5; Luka 13:11). Kiakili, Shetani huwapotosha watu katika makosa, akifundisha mafundisho ya uongo (1 Timotheo 4:1). Anatia shaka na kuwaweka wasioamini kupofushwa kiakili kwa ukweli wa kiroho na injili (2 Wakorintho 4:3-4). Yeye hupanga vikengeusha-fikira na kukaza mkanganyiko unaowafanya watu watende jambo kwa haraka, bila sababu, na kwa upumbavu. Kiroho, yeye huchukua kila nafasi ya kulinyakua Neno la Mungu lililopandwa moyoni mwa mtu (Mathayo 13:19).

Ibilisi anatamani kuwashambulia waumini pia (Luka 22:31-32). Atajaribu kuwafanya waumini wasimfuate Kristo ili kuwaepusha na kusudi lao kuu la kuleta utukufu kwa Mungu na kuendeleza makusudi na mipango yake. Ikiwa Shetani anaweza kusababisha upendo wetu kwa Kristo kupoa (Ufunuo 2:4) au kutufanya tuache kupendana sisi kwa sisi (Yohana 13:34-35), basi tunapoteza ushuhuda wetu mbele ya ulimwengu na kumchukiza Baba yetu wa mbinguni. Ikiwa Shetani anaweza kutushawishi katika uraibu kama vile buradani, ngono, au ponografia, basi anatuingiza katika utumwa wa dhambi ili tusiweze kuwasiliana na Mungu.

Kwa muhtasari, kazi za Shetani ni kupinga kazi ya Mungu. Kama muuaji, Shetani anafanya kazi dhidi ya Mungu, ambaye ni Uzima. Kama mwongo, Shetani anafanya kazi dhidi ya Mungu, ambaye ni Kweli. Katika maisha ya wasioamini, kazi ya Shetani ni kuwazuia wasije kwenye imani ya wokovu katika Kristo, na matokeo yake ni kwamba watapata kifo cha pili (Ufunuo 20:14-15). Katika maisha ya waumini, kazi ya Shetani ni kuwajaribu kutenda dhambi na hivyo kufifisha ufanisi wao kwa Kristo katika ulimwengu huu.

Bahati nzuri kwetu ni kuwa, Yesu Kristo alikuja kuharibu kazi za Shetani. Wakati wa kukamatwa na kusulubiwa kwake ulipokaribia, Yesu alisema, “Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje (Yohana 12:31). Msalabani Yesu alitimiza mambo mengi ya ajabu. Alichukua adhabu ya dhambi zetu na kutupa haki yake. Kwa hiyo, Shetani hana uwezo juu ya hatima ya milele ya waumini katika Kristo. Sio kwamba Shetani hawezi kumjaribu Mkristo kufanya dhambi na kufanikiwa wakati mwingine- ni kwamba kifo cha Yesu kilibeba ghadhabu yote ya Mungu dhidi ya dhambi hiyo, na Mungu hashikilii dhambi dhidi ya Mkristo (Warumi 8:1).

Sio tu kwamba kifo cha Yesu kiliharibu kazi za Shetani kuhusiana na hatima yetu ya milele, bali kilitoa utakaso wetu binafsi. Waumini wana karama ya Roho Mtakatifu ambaye anakaa ndani yao na kuwaongoza katika kufanana na Kristo. Roho huwatia muhuri wale wanaomwamini Kristo, na Shetani hawezi kuwaondoa katika ahadi Zake (Waefeso 4:30).

Katika wema wake, Bwana pia ametupa silaha za kiroho ili kupigana na Shetani (Waefeso 6:10-18). Ibilisi anaweza kutuletea mambo mengi, lakini, tukijiweka tukiwa tumevaa silaha za Mungu, vita vitakuwa rahisi zaidi. Na lazima tumuelewe adui yetu na kutambua anapokaribia: “Kwa maana hatuachi kuzijua hila zake” (2 Wakorintho 2:11). Muhimu zaidi, ni lazima tujue nguvu na ulinzi wetu ziko wapi na kumwamini “mkamilishaji wa imani” (Waebrania 12:2), ndiye pekee anayeweza kuharibu kazi za Shetani kwa kweli.

EnglishRudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je! Kazi za Shetani katika 1 Yohana 3:8 ni zipi?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries