settings icon
share icon
Swali

Je, Mungu ana mpango nami?

Jibu


Mipango mingi ya Mungu imeelezewa kwa undani katika Biblia. Ana mipango kwa mataifa, makundi ya watu, na kwa watu binafsi. Isaya 46:10-11 inaelezea kwa ufupi kile ambacho Mungu anataka tujue kuhusu mipango yake: “Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote. Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye; kutoka nchi ya mbali, mtu atakayetimiza kusudi langu.Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza; lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda.” Ni jambo moja kutambua kwamba Mungu ana mpango mkubwa kwa ulimwengu; na ni jambo lingine kabisa kutambua kwamba Mungu ana mpango maalum kwa maisha ya kila mtu.

Maeneo mengi katika maandiko yanaonyesha kwamba Mungu ana mpango maalum kwa kila binadamu. Mpango huu unaanza kabla hatujazaliwa. Bwana alimwambia Yeremia, “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa” (Yeremia 1:5). Mpango wa Mungu haukuwa wa kurekebisha,bali jibu kuhusu kuzaliwa kwa Yeremia. Ulitangulia, ukiashiria kuwa Mungu alimuumba mtoto huyu wa kiume ili kutimiza mpango wake. Daudi anathibitisha ukweli huu: “Maana wewe ndiye uliyeniumba mtima nami, Uliniunga tumboni mwa mama yangu” (Zaburi 139:13). Watoto ambao hawajazaliwa si ajali. Wameumbwa na Muumba wao kwa madhumuni yake. Hii ndio sababu moja inafanya uavyaji mimba ni makosa. Hatuna haki ya kuidharau mipango ya Mungu na kuvunja kazi ya Mungu kwa kumuua mtoto ambaye yuko katika mchakato wa kuumbwa.

Mpango wa Mungu kwa kila binadamu ni kwamba kila mmoja amjue na kukubali kujitoa kwake kwa wokovu (2 Petro 3:9). Alituumba tuwe na ushirika Naye, na tunapokataa upatanisho anaopeana, tunakwenda kinyume na mpango wake kwetu. Zaidi ya wokovu, Mungu pia alipanga kazi nzuri kwa kila mmoja wetu kulingana na vipawa vyetu, nguvu, na fursa (Waefeso 2:10). Alipanga mahali na wakati ambao kila mmoja wetu atazaliwa (Matendo 27:6; Zaburi 139:16). Ikiwa anajua idadi ya nywele kichwani mwetu, basi anatujua vizuri zaidi kuliko tunavyojijua sisi wenyewe (Luka 12:7). Anafahamu vipawa, vipaji, nguvu, na udhaifu ambao alitupa, na anajua jinsi tunavyoweza kuvitumia vizuri ili kufanya athari ya milele. Anatupa fursa ya kuhifadhi hazina mbinguni ili kwamba, kwa milele yote, tunaweza kufarahia thawabu yake (Marko 9:41; Mathayo 10:41-42).

Mpango wa Mungu kwa kila mtu kwa ujumla umetajwa katika Mika 6:8: “Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!” Mpango wake unalenga uhusiano badala ya majukumu. Tunapotembea katika Roho (Wagalatia 5:16,25), tukifurahia uhusiano wa upendo na Bwana, matendo yetu yanadhihirisha huo ukaribu. Kumfurahisha Mungu ndio furaha yetu. Mpango wake unafunuliwa kwa asili kadri tunavyokua katika imani, kukua katika maarifa, na kutii kwa kila tunachoelewa. Tunapotii mipango yake kwa watoto wake, tunagundua mpango wake wa kipekee kwa kila mmoja wetu.

Tunajua kwamba mpango wa Mungu kwa wale wanaomjua Yeye ni pamoja na kuwafikia wengine na habari njema ya wokovu (Mathayo 28:19; 2 Wakorintho 5:20). Mpango wake ni kuwafanya watoto wake wafanane na Yesu Kristo (Warumi 8:29). Anataka tuongezeke katika neema na maarifa (2 Petro 3:18). Anataka tuwapende Wakristo wenzetu kama vile Yeye anavyotupenda (Yohana 13:34). Tunapofuata neno lake,tutagundua vipawa vyetu vya kiroho na uwezo ambao unatufaa kumtumikia kwa njia ya kipekee (2 Wakorintho 12:4-11). Mpango wa Mungu unafunuliwa katika maisha yetu tunapotumia vyema tulichonacho kwa utukufu wake (1 Wakorintho 10:31).

Mara nyingi sisi tunakosa uvumilivu wakati tunapohangaika kujua kuhusu mpango wa Mungu katika maisha yetu. Lakini sio ngumu kama tunavyofikiria. Mpango wa Mungu kwetu unafichuliwa kidogo kidogo tunapomfuata,na mpango wake unaweza kuonekana tofauti katika misimu tofauti ya maisha.Mwanamke mdogo anaweza kumwomba Mungu amwongoze katika mpango wake na anaamini kwamba chuo kikuu ni sehemu ya mpango huo.Lakini kabla ya kumaliza chuo kikuu, anaugua na lazima atumie miaka miwili ijayo katika nyumba ya kupumzika na kupona. Je! Yupo nje ya mpango wa Mungu sasa? Hapana, ikiwa ameeka moyo wake kumtii Mungu. Katika nyumba iyo ya kupumzika na kupona, anakutana na kijana ambaye anakuwa mume wake. Wote wanampenda Bwana na wanatamani kumtumkia na kuamini kwamba mpango Wake kwao ni kueneza injili. Wanaanza maandalizi, lakini katikati ya mafunzo, anapata mimba yenye iko katika hatari kubwa. Je! Walikosa mpango wa Mungu? Je! Bwana aliwaacha? Hapana. Kwa sababu ya uzoefu wao wa kumlea mtoto mwenye mahitaji maalum, wako na uwezo wa kuhudumia familia zingine zenye mahitaji kama hayo. Uwanja wao wa misheni unaonekana tofauti sana na ule waliokuwa wameufikiria, lakini ni mpango wa Mungu kwao. Wanaweza kutazama nyuma na kuona mkono wake katika kila hatua yao ya maisha.

Mpango wa Mungu mara nyingi hauna njia nyepesi ya kufikia lengo lililo wazi. Mpango wake unahitaji safari, na safari hiyo inaweza kuwa na mizunguko, mizunguko ya ghafla, na mizunguko yenye kuleta utata. Lakini ikiwa mioyo yetu imeelekezwa kumtii katika yote tunayojua kufanya, basi tutakuwa katikati ya mapenzi yake kila hatua ya safari.

EnglishRudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je, Mungu ana mpango nami?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries