settings icon
share icon
Swali

Kwa nini Mungu alimruhusu Sulemani kuwa na wake na Masuria 1,000?

Jibu


Wafalme wa Kwanza 11:3 inasema kwamba Sulemani “alikuwa na wake 700 mabinti wa uzao wa kifalme, na masuria 300.” Ni wazi kwamba, Mungu ‘alimruhusu’ Sulemani kuwa na wake hao, lakini kuruhusiwa haimanishi kuwa na kibali. Maamuzi ya Sulemani ya ndoa yalikuwa ukiukaji wa Sheria ya Mungu, na kulikuwa na matokeo.

Mwanzoni mwa maisha yake, Sulemani alianza vizuri sana, akisikiliza shauri la baba yake, Daudi, kama lilivyoandikwa katika 1 Wafalme 2:2-3, “ Hivyo uwe hodari, jionyeshe kuwa mwanaume, shika lile Bwana Mungu wako analokuagiza: Enenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Musa, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote uendako.” Unyenyekevu wa mapema wa Sulemani unaonyeshwa katika 1 Wafalme 3:5-9 anapaoomba hekima kutoka kwa Bwana. Hekima ni maarifa yanayotumika: inatusaidia kufanya maamuzi yanayomheshimu Bwana na kukubaliana na Maandiko. Kitabu cha Sulemani cha Mithali kimejaa ushauri wa vitendo wa jinsi ya kumfuata Bwana. Sulemani pia aliandika Wimbo Ulio Bora, ambacho kinatoa picha nzuri ya kusudi la Mungu la ndoa. Kwa hiyo, Mfalme Sulemani alijua kilicho sawa, hata kama hakufuata njia hiyo bora kila wakati.

Baada ya muda, Sulemani alisahau ushauri wake mwenyewe na hekima ya Maandiko. Mungu alikuwa ametoa maagizo ya wazi kwa yeyote ambaye angekuwa mfalme: hakuna kukusanywa kwa farasi hakuna kuzidisha wake, na hakuna kukusanya fedha na dhahabu (Kumbukumbu 17:14-20). Amri hizi zilikusudiwa kumzuia mfalme asitegemee uwezo wa kijeshi, kufuata miungu ya kigeni, na kutegemea mali badala ya kumtegemea Mungu. Uchunguzi wa maisha ya Sulemani utaonyesha kwamba alivunja makatazo hayo yote matatu ya kimungu!

Hivyo, kuoa wake na masuria wengi kwa Sulemani kulivunja Neno la Mungu moja kwa moja. Kama vile Mungu alivyotabiri, “Kadri Solomoni alivyozidi kuzeeka, wake zake wakaugeuza moyo wake kuelekea miungu mingine, na moyo wake haukujitolea kikamilifu kwa Bwana Mungu wake” (1 Wafalme 11:4). Ili kuwafurahisha wake zake, Sulemani hata alijihusisha katika kutoa dhabihu kwa Milkomu (au Moleki), mungu aliyetaka matendo “ya kuchukiza” yafanywe (1 Wafalme 11:7-8).

Mungu alimruhusu Sulemani kufanya uamuzi wa kutotii, lakini uamuzi wa Sulemani ulileta matokeo yasiyoweza kuepukika. “Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, “Kwa kuwa hii ndiyo hali yako na hukushika Agano langu na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme kutoka kwako na kumpa mmoja wa walio chini yako” (1 Wafalme 11:11). Mungu alimwonyesha Sulemani rehema kwa ajili ya Daudi (mstari wa 12), lakini ufalme wa Sulemani hatimaye uligawanyika. Adhabu nyingine juu ya Sulemani ilikuwa vita na Waedomu na Waaramu (mistari ya 14-25).

Sulemani hakuwa mfalme bandia. Mungu hakumlazimisha kufanya lililo sawa. Badala yake, Mungu aliweka wazi mapenzi Yake, akambariki Sulemani kwa hekima, na kumtarajia mfalme atii. Katika miaka yake ya baadaye, Sulemani aliamua kutotii, na aliwajibika kwa maamuzi yake.

Inafundisha kwamba, kuelekea mwisho wa maisha ya Sulemani, Mungu alimtumia kuandika kitabu kimoja zaidi, ambacho tunapata katika Biblia. Kitabu cha Mhubiri hutupatia “hadithi iliyobaki.” Sulemani katika kitabu chote anatuambia kila jambo alilojaribu ili kupata utimizo mbali na Mungu katika ulimwengu huu, au “chini ya jua.” Huu ndio ushuhuda wake mweneywe: “Nikajikusanyia fedha na dhahabu, hazina za wafalme na za majimbo. Nikajipatia… nazo nyumba za masuria: vitu ambavyo moyo wa mwanadamu hufurahia” (Mhubiri 2:8). Lakini nyumba za masuria hazikuleta furaha. Badala yake “kila kitu kilikuwa ni ubatili, ni kukimbiza upepo; hapakuwa na faida yoyote chini ya jua” (mstari wa 11). Kwenye tamatizo la Mhubiri tunapata shauri hili lenye hekima: “Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa: Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu” (Mhubiri 12:13).”

Si mapenzi ya Mungu kamwe kwamba mtu yeyote atende dhambi lakini Yeye huturuhusu kufanya maamuzi yetu wenyewe. Hadithi ya Sulemani ni somo lenye nguvu kwetu kwamba kutotii hakuzai matunda. Haitoshi kuanza vizuri; lazima tutafute neema ya Mungu ili kumaliza vyema pia. Maisha bila Mungu ni njia isiyo na mwisho. Sulemani alifikiri kwamba kuwa na wake na Masuria 1,000 kungemletea furaha, lakini raha yoyote aliyopata haikustahili gharama aliyolipa. Sulemani mwenye hekima alifikia hitimizo kwamba maisha yake ya kujifurahisha hayakuwa na “maana” (Mhubiri 12:8), na kitabu cha Mhubiri kinamalizia kwa onyo kwamba “Mungu ataleta hukumuni kila kazi” (mstari wa 14).

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Kwa nini Mungu alimruhusu Sulemani kuwa na wake na Masuria 1,000?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries